#7 NAYE APANDAYE MBEGU ZA FITINA KATI YA NDUGU
VITU SABA AMBAVYO NI CHUKIZO KWAKE BWANA
Soma Mithali 6:16-19 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.
Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
Tunamaliza masomo yetu kuhusu vitu vinavyomchukiza Bwana. Kitu cha mwisho kinachomchukiza Bwana ni yule apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
NAYE APANDAYE MBEGU ZA FITINA KATI YA NDUGU
Inanishangaza ninapotazama katika orodha ya Mithali 6 kuhusu vitu ambavyo ni chukizo kwake Bwana. Vitatu vinahusu usemi wetu, mazungumzo yetu yaani ulimi wetu. Neno "fitina" linatumiwa zaidi ya mara 86 katika Biblia. Maneno mengine yanayofanana na neno hili ni "mafarakano, ugomvi, uadui, kutokubaliana, ugawanyiko, kutokuwa na umoja na mengine. Kwa hiyo kitu kinachomchukiza Bwana, ni mtu apandaye mbegu kama hizi kati ya ndugu. Labda ni ndugu wa familia, ndugu kanisani, kazini, mtaani au mahali po pote. Ina maana gani kupanda mbegu za fitina? Inamaanisha kukuza shida, kuwa "mlezi" wa, kuumba matatizo kati ya watu na kusabibisha hali ya ubaya au shida kati ya watu.
Kwa mkulima, kazi ya kupanda mbegu siyo kazi zinazofanywa ovyo ovyo. Mkulima kwanza anatafuta "mahali" pa kupanda, pia anatafuta "aina ya mbegu" ya kupanda. Yule mkulima analima udongo, na labda kuweka mbolea, kutengeneza mistari na mifereji halafu kupanda mbegu. Vile vile kwa mtu ambaye anapanda mbegu za fitina. Mtu hawezi moja kwa moja kupanda mbegu za fitina. Anapaswa kusikiliza mazumgumzo ya watu, kupima maneno yao na kidogo kidogo kuanza kupanda mbegu za uovu. Katika kundi la watu, yule mwovu anamtafuta mdhaifu kwanza kuanza kupanda zile mbegu za fitina. Warumi 16:17 inasema Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao. Waefeso 4:1-3- Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Sisi wengi tunajua na labda tumekariri Wagalatia 5:22-23 kuhusu "tunda la roho." Lakini kabla ya kuorodhesha matunda hayo, mistari inayotangulia inataja mambo ya kidunia au ya kimwili ili kumaanisha wafuasi wa shetani. Wagalatia 5:19-21 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Angalia maneno ya "uadui, ugomvi, fitina na faraka." Katika orodha ya vitu 15 vinavyoorodheshwa, nne vinahusu mambo ya kutokubaliana au fitina. Mithali 16:28- "Mtu mshupavu huondokesha fitina; Na mchongezi huwafarakanisha rafiki."
Tukitafuta sababu kwa nini mtu anapanda fitina, tunaweza kutaja sababu mbali mbali. Kiburi ni kitu kikubwa. Kiburi kinasema "mawazo yangu ni bora kuliko yako." Wafilipi 2:3- "Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake." Pia, ubinafsi unaweza kuchangia. Watu wanataka njia zao na mapendekezo yao.
Tuwe watu ambao wanajengana, siyo kutengana wala kutenganisha. Tusiwe watu ambao wanapanda mbegu za fitina kati ya ndugu. Tuwe watu wa JASHO. Jengana, angaliana, saidiana, heshimiana na ombeana
Ombi:
Mungu Bwana, naomba msamaha kwa jinsi ninavyochangia kupanda mbegu za fitina kati ya ndugu zangu. Naomba unisamehe. Nisiwe mtu ambaye anafanya vitu vinavyokuchukiza wewe Bwana. Nisaidie kuwa mpatanishi wala siye mtenganishi. Amina.