#6 SHAHIDI WA UWONGO ASEMAYE UONGO

written by Mary Smith, Audio by Tina Omolo

VITU SABA AMBAVYO NI CHUKIZO KWAKE BWANA


Soma Mithali 6:16-19 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. 

Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu. 

   

Tunaendelea kujifunza kutoka Mithali 6 kuhusu vitu saba ambavyo ni chukizo kwake Mungu. Leo tunaendelea na namba sita, shahidi wa uwongo asemaye uongo. Bila shaka sisi sote tumewahi kuguswa na jambo hili, na labda kuumizwa kwa sababu ya uwongo wa mwingine.


SHAHIDI WA UWONGO ASEMAYE UONGO


Katika vitu saba ambavyo Mungu anavichukia, kumbe, mbili vinahusu uwongo. Mithali 6:17 inataja "ulimi wa uongo" na sasa katika mstari wa 19 tunakuta "shahidi wa uongo." Katika Amri kuu za Mungu tunakuta " Usimshuhudie jirani yako uongo." Tunaona jambo hili katika Kutoka 23:1-2, Mambo ya Walawi 19:12 na mara 117 zaidi katika Neno la Mungu. Je, hii ilikuwa shida katika historia au ni shida hata siku hizi? Nafikiri wote watajibu"ndiyo, ni shida hata leo." Mithali 25:18 unasema " Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo "Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali." Ni kweli tunaposikia kuhusu mtu ambaye anasema uwongo ni kana kwamba tumepigwa na maneno yao, tumekatwa na kuumizwa na uwongo wao. Wangapi wameteswa au kuwekwa gerezani kwa sababu ulikuwa shahidi wa uongo? Hata Yesu aliwaambia askari wa Warumi walipouliza "na sisi tufanyeje?" Yesu aliwajibu katika Luka 3:14 "Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; Mithali 12:17 unasema "Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila"

   

Wengine labda wanaweza kujitetea na kubadilisha maneno au ushuhuda wao kidogo tu. Lakini, hata kidogo ni uwongo. Kumbuka Mathayo 26:59-61 "Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;  wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi.  Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Mashahidi yakabadilisha maneno ya Yesu, kidogo tu. Wakasema uwongo. Nyoka, bustani ya Edeni, alimshawishi Hawa kwa kubadilisha maneno ya Mungu, kidogo tu. Kuongeza au kupunguza maneno ya mwingine, bado ni uwongo.

   

Maneno yetu yanaweza kuwajenga wengine au kuwakata na kuwaumiza. Kitabu cha Yakobo mlango wa tatu unatueleza sana kuhusu hatari ya ulimi. Yakobo alikuwa mchungaji wa kanisa la Yerusalemu. Bila shaka katika ushirika wa kanisa lake aliona shida zilizotokea kwa sababu ya shida za ulimi na mashahidi wa uwongo. Katika kitabu cha Yakobo anasema ulimi ni kama sumu, ni moto na uovu. Tena hakuna mtu ambaye anayeweza kuufuga. Tena anatuambia "haifai" kwa laana na baraka yatoke mdomo moja. Fikiria ni unafiki wa namna gani kwa Mkristo kuimba na kumsifu Mungu halafu kuwa shahidi wa uwongo asemaye uongo. 

   

Neno hili "shahidi" linamaanisha mtu ambaye mwenyewe ameona kitu au amesikia kitu. Tusiwe watu ambao wanabadilisha ukweli wa matokeo fulani kwa kusema uwongo. Tuwe mashahidi wa ukweli. Zaburi 19:14 inasema "Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Bwana."

Ofisini, nyumbani,mtaani na hata kanisani, ni rahisi kujiunga na wengine katika kuwasengenya wengine. Sisi kama Wakristo, tuwe mfano bora. Tusimchukize Bwana kwa kuwa mashahidi wa uwongo.


Ombi:

Bwana Yesu, naomba unisamehe pale nilipokuwa shahidi wa uwongo asemaye uwongo. Naomba unisaidie kuwa shahidi wa ukweli kila mara. Nisibadilishe maneno ya wengine, wala kuongeza au kupunguza maneno ya wengine. Maneno ya kinywa changu yapate kibali mbele zako. Amina.