#4 MOYO UWAZAO MAWAZO MABAYA
Soma Mithali 6:16-19 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
Tunaendelea na masomo ya vitu saba ambavyo ni chukizo kwa Bwana. Katika masomo mengine tumeshajifunza kuhusu macho ya kiburi, ulimi wa uongo na mikono imwagayo damu isiyo na hatia. Leo tunasoma mstari wa 18. Mungu anachukia Moyo uwazao mawazo mabaya.
MOYO UWAZAO MAWAZO MABAYA
Neno la Mungu linataja neno "moyo" mara 826. Tunaweza kujua moyo wa Mungu kwa kusoma Neno lake. Tunaweza kuwa na moyo safi, moyo wenye nguvu, moyo dhaifu, moyo ya kumpendeza Mungu na moyo uwazao mawazo mabaya. Yeremia 17:9 Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mithali 6:12 unasema "Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu" na unaendelea kumweleza mtu yule katika mstari wa 14 unasema "Mna upotofu moyoni mwake hutunga uovu daima. Mawazo na mafikira yanaanza moyoni. Mithali 23:7 "Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo." Neno "nafsini" mara nyingi linatafsiriwa "moyo." Tena katika Mathayo 5:27-28 Yesu anawaonya watu kuhusu "uzinzi" wa moyo. Tukitaka moyo unaompendeza Mungu, tunapaswa kujifunza jinsi ya kutawala mioyo yetu na kuilinda. Mithali 4:23 unatuambia "kulinda moyo kuliko yote uyalindayo." Kwa sababu Yeremia 17 unatuambia mioyo yetu imejaa udanganyifu na ugonjwa wa kufisha, lazima tujue jinsi ya kulinda moyo na kuutawala. Yesu anawaeleza watu katika Marko 7:18-19 siyo vitu vya nje vinavyoleta shida, lakini ni vitu vya moyoni.
Tusipolinda mioyo yetu na mawazo yetu, tunajiweka hatarini. Moyo na mawazo yanaenda pamoja na sambamba. Tunapoanza kuwaza mawazo mabaya, II Wakorintho 10:5 unasema " tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu." Tukianza kuwaza sana moyoni kuhusu waume zetu au wengine pia, tunapaswa moja kwa moja kukataa mawazo haya. Tusiruhusu mioyo yetu kuwaza mawazo mabaya yanayomchukiza Bwana. Tena tujifunze jinsi ya kuomba kama Daudi alivyoomba katika Zaburi 139:23-24 "Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele."
Tena Zaburi 51:10 "Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu."
Kutawala mioyo yetu na mawazo yetu ni kazi ya kila siku. Tunapokasirika, ni rahisi kuruhusu mawazo ya kulipiza kisasi yakue na kuota mizizi katika moyo. Waebrania 12:15-unasema "shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua." Tunapoumizwa na maneno au matendo ya familia, marafiki au wenzetu kazini, tusiliruhusu shina la uchungu kuotesha mizizi mioyoni mwetu. Tukitaka kumpendeza Mungu, tuwe tayari kujinyenyekeza na kuja mbele za Mungu na kuomba msamaha. Tumwombe Mungu kuchunguza mioyo yetu kila siku ili tuweze kuondoa dhambi zinazojificha moyoni. Tuwe radhi kuteka nyara mawazo mabaya kama tunavyoambiwa katika II Wakorintho 10:5-"tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo." Mwishowe Waefeso 4:31 unasema " Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya." Mambo hayo yote yanaanza katika moyo. Linda moyo wako usikutwe na moyo uwazao mawazo mabaya.
Ombi:
Bwana Yesu, mimi ni mwenye dhambi. Naomba unisamehe ninapowaza vibaya kuhusu wengine. Naomba unisaidie kutawala moyo na mawazo yangu. Chunguza moyo wangu, uyajue mawazo yangu. Nisaidie kukupendeza wewe na yote nafanyayo na yote nawazayo. Amina