#1 MACHO YA KIBURI

written by Mary Smith, Audio by Tina Omolo

Soma Mithali 6:16-19 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.  Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;  Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;  Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu. 


Tunasoma katika sehemu hii ya Mithali, kuhusu vitu vilivyo chukizo kwake Mungu. Katika kitabu cha Mithali tunajifunza kuhusu Baba ambaye anamshauri mwanawe. Kutoka katika mlango wa kwanza tunakuta maneno "mwanangu" na "sikiliza". Akina Baba na Mama wote wanataka watoto wao kufaulu, na kusikiliza shauri linalofaa. Mungu vile vile anataka sisi kufaulu na pia kumpendeza yeye. Tumepewa Neno la Mungu, Biblia, ili tuweze kujifunza, kusikiliza, kurekebisha njia zetu na kujua moyo wake Mungu. Ikiwa wewe ni Mkristo, Mungu anatuambia wazi vitu ambavyo ni chukizo kwake. Tuangalie vitu hivi kimoja baada ya kingine.


MACHO YA KIBURI

Kitu cha kwanza kilichotajwa na Mungu katika Mithali 6:17 ni "Macho ya Kiburi." Kamusi inatuambia maana ya kiburi kumaanisha "kujifikiria kama mtu bora kuliko wengine, kujifikiria kama mtu muhimu, mwenye cheo." "Macho ya Kiburi" inamaanisha mtu ambaye anawaangalia wengine kana kwamba hawana cheo au umuhimu machoni pao. Labda ni tajiri ambaye anamdharau maskini, au mwenye elimu kutomheshimu yule ambaye hajasoma. Labda ni mtu ambaye anafikiri kabila lake ni bora kuliko kabila la mwingine. Yeremia 9:23- "BWANA asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake."

   

Kiburi kinajitokeza katika sehemu zote za maisha. Mungu anasema anaichukia. Haina mahali maishani pa Mkristo. Kwanza, tunaona hii ilikuwa shida kubwa ya Ibilisi. Isaya 14:13-15 inatueleza kuhusu Ibilisi na jinsi alivyotupwa chini kutoka mbinguni kwa sababu ya kiburi chake. Kuna mistari zaidi ya 153 kuhusu kiburi katika Biblia. Mithali 8:13 unasema "kiburi na majivuno na njia mbovu na kinywa cha ukaidi pia nakichukia." Mithali 16:18 unasema "kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko." Ukitaka kuwa mbali na njia za Mungu, uwe na kiburi. Yakobo 4:6 unasema "Mungu huwapinga wajikuzao." Yesu mwenyewe alikuwa mfano wetu wa unyenyekevu, kinyume cha kiburi. Tena Yakobo anatuonya sisi sote kanisani tusiwe na kiburi. Yakobo 2 inatuambia tusiwaheshimu matajiri na kumdharau maskini. Kiburi inasema "nitamfanyia yeye tofauti kwa sababu ya utajiri wake." Jamani, kiburi haifai. 

I Yohana 2:16 unatuambia "kiburi cha uzima havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia".

   

Tukitaka kuwa watu ambao wanampendeza Mungu, LAZIMA tujishushe badala ya kujivunia. Kama tulivyosema, unyenyekevu ni kinyume cha kiburi. Mungu anaichukia kiburi lakini anapenda unyenyekevu. Yakobo 4:10 "Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua."


I Petro 5:7- "Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake." Sisi sote tunataka kuheshimiwa na kuhesabiwa kuwa watu wa thamani. Mungu anatuthamini sisi. Tumruhusu Bwana kutuinua kwa wakati wake. Tusijivunie au kutowaheshimu wengine kwa sababu ya macho yetu ya kiburi.


Ombi:

BWANA YESU, nakuja mbele zako kwa shukrani. Nashukuru kwa Neno lako linalonifundisha na kunionya. Bwana, naomba unisamehe kiburi changu. Naomba unisaidie kutambua kiburi changu na dhambi zangu. Unisaidie kujinyenyekeza mbele zako na mbele za wengine. Nisiwe na macho ya kiburi bali nisaidie kuwa na macho ya huruma, rehema na unyenyekevu. Naomba LEO niwe mfano wa upendo wako. Asante Mungu kwa mwanako aliyejinyenyekeza mpaka msalaba kwa ajili yangu. Katika jina la Yesu Kristo. Amina