#3 MIKONO IMWAGAYO DAMU ISIYO NA HATIA
Soma Mithali 6:16-19
Somo hili linaendelea kuchunguza sehemu hii ya Biblia. Tayari tumeshajifunza kuhusu macho ya kiburi na ulimi wa uongo katika mstari 17. Tumalize mstari huu kwa kujifunza kuhusu kitu cha tatu ambacho Mungu anakichukia.
MIKONO IMWAGAYO DAMU ISIYO NA HATIA
Katika historia ya dunia tunakuta mazoea mbali mbali ambayo siku hizi hatuwezi kuamini. Kwa mfano, siku hizi hatuna watumwa kama zamani. Hatuoni kabila moja linalotawala kabila lingine na kuwauza kama mali katika biashara. Hatuoni familia wanaouzwa kwa sababu ya deni zisizolipwa. Pia katika historia ya dunia, tunaona mazoea ya kutoa sadaka au dhabihu ya watu kwa miungu mbali mbali. Mazoea ya kutoa watoto, hasa mtoto wa kwanza, ilifanyika, tena sana. Katika Agano la Kale, tunasoma Mungu alichukia mazoea haya ya kumwaga damu isiyo na hatia. Waisraeli walikatazwa kujiunga na sadaka kama hizo. Mambo ya Walawi 18:21 Nawe usitoe kizazi chako chochote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi Bwana. Kumbukumbu la Torati 12:31-Kamwe msimwabudu Bwana Mungu wenu kwa njia wanayoabudu miungu yao, kwa sababu katika kuabudu miungu yao, wanafanya aina zote za machukizo anayoyachukia Bwana. Hata huwateketeza wana wao na binti zao kwa moto kama kafara kwa miungu yao.” Lakini Waisraeli walitaka kufanana na mataifa mengine. Ghadhabu ya Mungu iliwaka kwa sababu hiyo.
II Wafalme 17:17 "Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni." Zaburi 106:37-38 "Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu." Siku hizi tunaangalia mazoea haya kwa kushangaa na kutikisa kichwa na kutoamini kwamba watu waliweza kufanya mambo kama hayo. Kumwaga damu isiyo na hatia ni chukizo kwa Bwana.
Na sisi je? Mataifa mangapi yamekubali kuwaruhusu wasichana na akina mama kutoa mimba? Wanasema ni "haki" yao. Sayansi yenyewe inatuambia moyo wa mtoto tumboni mwa mama unaanza kupiga mapigo baada ya siku 21 ya mwanzo wa uja uzito. Mtoto yu hai. Lakini, watu wa dunia wanatoa sababu za "Muda haufai, uchumi haufai, sitaki mtoto mwingine" n.k. Yule mtoto ambaye yu hai tumboni, hana hatia. Hastahili kuuawa kwa sababu yo yote. Sisi wafuasi wa Yesu tunapaswa kusimama dhidi ya uovu huu. Ikiwa ni binti zetu, dada zetu au rafiki zetu, tunapaswa kushikamana na Neno la Mungu na kuwashauri wengine kwamba ni dhambi kumwaga damu isiyo na hatia. Hatuwezi kukaa kimya na haifai kukaa kimya. Tena katika Mambo ya Walawi 20:4-5, Mungu anaeleza wazi itakuwaje kwa wale ambao wanakubali kumwaga damu isiyo na hatia. "Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue; ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na Moleki, watengwe mbali na watu wao." Ikiwa wewe mwenyewe umewahi kutoa mimba. Ujue ya kwamba, Mungu wetu ni Mungu wa rehema na msamaha. I Yohana 1:9 unatuambia tukiziungama dhambi, atatusamehe. Unaweza kumwomba Mungu akusamehe sasa hivi. Nakushauri utafute ushauri wa Mkristo mwaminifu mpevu ili akuonyeshe jinsi ya kumpokea Yesu kama Mwokozi na Bwana wa maisha yako ikiwa hujawahi kufanya hivyo.
Mfano mwingine ni Kaini na Abeli katika kitabu cha Mwanzo. Abeli hakufanya kosa lolote. Lakini hasira ya Kaini ilimshika mpaka alimwuua mwenzake. Katika Mithali 1:10-15 tunaona kundi la watu ambao wanatarajia kuwaua watu ili kuchukua mali yao. Wengine wanajaribu kuwatetea wale ambao wamewaua wengine. Katika Amri za Mungu, anatuambia wazi "Usiue". Tunaona katika Agano Jipya jinsi watu walivyomwaga damu ya Stefano, Yohana Mbatizaji, wafuasi wa Yesu na Yesu mwenyewe. Hawakufanya kosa la kustahili kuuawa. Ingawa hawakukuwa na hatia, damu yao ilimwagika.
Ombi:
Mungu Baba, naomba unisaidie kusimama imara dhidi ya uovu. Nisaidie kuwashauri wengine kutoka katika Neno lako tu. Unisaidie kuamini na kufanya Neno lako, hata ikiwa napaswa kusimama dhidi ya mawazo ya wengine. Katika jina la Yesu Kristo. Amina