#2 ULIMI WA UWONGO
Soma Mithali 6:16-19 16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
Wakati uliopita tulianza kujifunza kuhusu vitu ambavyo ni chukizo kwake Mungu. Katika orodha ya Mithali 6:16-19, tulijifunza kuhusu kitu cha kwanza, macho ya kiburi. Leo tunaangalia kitu cha pili, ulimi wa uwongo.
ULIMI WA UONGO
Neno la Mungu linataja "uwongo" mara 166. Ikiwa inatajwa mara nyingi kama hivyo, bila shaka ni muhimu. Tena, kumbuka tupo katika masomo ya vitu ambavyo Mungu anavichukia. Hata katika Amri kumi za Mungu, tunakuta "Usimshuhudie jirani yako uwongo". Siku hizi, watu wanaona ni jambo ndogo kusema uwongo. Wengine wanasema "ilikuwa uwongo mdogo tu, uwongo mwepesi." Lakini, sisi ambao ni wafuasi wa Yesu, tunapaswa kuhakikisha hatusemi uwongo. Mithali 12:22 unasema "Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake." Zaburi 34:13 "Uuzuie ulimi wako na mabaya na midomo yako na kusema hila." Ndoa ngapi zimeharibika kwa sababu mmoja au mwingine anasema uwongo? Marafiki wangapi wameachana kwa sababu ya uwongo? Sijui mara ngapi nipo pamoja na wengine na mtu moja anajibu simu na kusema "ndiyo, nipo njiani" na kumbe, anasimama pale pale na kuongea! Uwongo! Pia katika biashara nimeshuhudia uwongo mwingi. Wanasema itakuwa tayari siku fulani wakati ambapo wanajua haiwezekani. Mungu anachukia uwongo.
Katika kitabu cha I Wafalme 21:1-16 tunasoma kuhusu Nabothi. Mfalme Ahabu alitaka kununua shamba lake na alikataa. Yezebeli aliwalipa watu kusema uwongo ili aweze kuchukua shamba lile. Nabothi aliuawa kwa sababu ya ushahidi wa uwongo. Yesu Kristo aliuawa kwa sababu ya ushahidi wa uwongo wa Mafarisayo. Baada ya kufufuka kwake Yesu, maaskari walilipwa kusema mwili wa Yesu uliibwa na wafuasi wake. Uwongo unaangamiza vitu vingi na huharibu maisha ya wengi.
Kinyume cha uwongo ni ukweli. Ukweli ni Yesu. Yohana 14:6 "Yesu alisema "Mimi ndimi njia, na kweli na uzima." Wakolosai 3:9-10 inasema "Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawa sawa na mfano wa Muumba wake." Tulipookoka, tumevaa maisha mapya. Tunapaswa kuacha mambo ya dunia hii na kuvaa mambo mapya. Wakolosai 4:6 unatuambia "Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu." Tuwe kama mwandishi wa Zaburi 141 mstari wa 3. Yeye alimwomba Mungu maneno haya - "Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu." Tupo vitani. Neno la Mungu linatuambia kuwa tayari kupinga hila za shetani. Waefeso 6:14 inatuambia "mmejifunga kweli kiunoni." Maneno yetu yaaminike. Maneno yetu yategemewe. Mathayo 5:37 inasema "Maneno yenu yawe ndiyo, ndiyo; siyo siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu."
Maombi yetu yawe kama Zaburi 39:1- "Nalisema, nitazitunza njia zangu. Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu."
Kuomba:
Mungu Baba, naomba unisaidie kutosema uwongo. Weka askari kinywani kwangu. Niwe mtu wa kweli. Nisamehe kwa kusema uwongo. Naomba unisaidie kukupendeza kwa usemi wangu. Katika jina la Yesu, Ukweli wetu, Amina.