#2 Utangulizi Maelezo kwa Mwalimu
Utangulizi...
habari
Maelezo Kwa Mwalimu au Mshauri:
Mistari hii imepangwa katika vifungu vinavyomaanisha tabia za tunda la Roho. Kwa kusoma vifungu vya mistari pamoja na kujibu maswali utaelewa vizuri zaidi maana ya kila tabia ya tunda la Roho mtakatifu.
Unaweza kutumia kijitabu hiki kwa kusaidia katika njia hizi tatu:
Wewe binafsi, kumjua Mungu zaidi, kupata hekima mwenyewe, kujua jinsi ya kuishi maisha yako.
Kumshauri mwenzako mwingine
Kuwa Mafundisho katika kikundi cha wanawake. Kila wiki kwenye kikundi chagueni tabia moja wa kusoma halafu jibu maswali pamoja kwa mazumgumzo. Kuna seti moja ya maswali inayotumika tena na tena.
Hatua 7 za kutumia Vifungu vya Mistari kuwa Mafundisho kwa Kikundi:
Omba na mtegemee Mungu kukufunulia maana ya vifungu upate kuvielewa vizuri.
Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi. (Zaburi 119:144)
Soma mistari yote katika somo moja
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu. (Zaburi 119:105)
Jibu maswali moja moja.
Chunguza mistari tu kwa majibu ya maswali. Majibu yatoke katika jinsi ilivyoandikwa hapo kwa Neno. Usimwache mtu yeyote kujibu kutokana na mawazo yake, yeye mwenyewe. Watu wajibu kutokana na jinsi Neno linavyosema hapo tu. Yaani, tumia mistari kuwa asili ya majibu yote. Biblia inasemaje?
Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. (2 Timotheo 2:15)
Fanya mjadala, yaani wanawake wote wajitahidi kujibu maswali kwa kutumia mistari ile iliyowagusa kila mmoja tofauti tofauti.
Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema. Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, siku ile ya Bwana inakaribia (Waebrania 10:24-25)
Kariri mstari mmoja ya kila kifungu cha mistari.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. (Zaburi 119:11)
Tumia mistari katika maisha yako, maisha ya familia yako, na maisha ya jamii zako.
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mikfundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. (Kolosai 3:16)
Maswali ya Kutumika
kwa kila tabia.
Tumia maswali hayo na kila tabia ya tunda la Roho inayofuata. Ni Sharti majibu yote yatokee kutoka katika mistari iliyoandikwa katika kifungu cha kila somo!
1. Vifungu vya somo vinatuambia nini kuhusu Mungu?
2. Vifungu vinatuambia nini kuhusu binadamu?
3. Taja baraka au ahadi za Mungu zinazoandikwa katika vifungu.
4. Taja maonyo au adhabu zinazoonekana.
5. Taja mafundisho ya kutii yanayoonekana.
6. Mnawezaje kumshuhudia mwingine kwa kutumia mistari hii?
7. Taja somo moja ambalo utajaribu kujitia au kutekeleza maishani.
Mafafanuzi juu ya Tunda la Roho
Soma Galatia 5:16-23, 16 Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. 19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, 20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. 22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. 24Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
Hapo mtume Paulo aliandika juu ya fikra au dalili za aina mbili zililizo tofauti sana.
Dalili za Kwanza ni Tamaa za Mwili: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, n.k.
Dalili za Pili ni Tunda la Roho: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi
Tamaa za mwili zikwepwe na Wakristo kwa kuwa:
Zinashindana na Roho Mtakatifu (m. 17)
Ni Dalili za watu wasioongozwa na Roho (m. 17)
Ukitembea na hizo tamaa, hutaurithi ufalme wa Mungu (m. 21)
Wakristo wameshasulibisha tamaa hizo katika Kristo—Zimekufa (m. 24)
Tunda la Roho linapatikana katika Wakrisoto pekee
Linakuja baada ya wokovu kwa uwezo wa Roho wa Mungu
Tukienenda na Roho Mtakatifu tutakuwa na tunda hili (mm. 16, 25).
Katika maisha ya Mkristo Tamaa za Mwili zitaendelea kupingana na Tunda la Roho. Lakini, katika Kristo unaweza kuzishinda! Si kwa nguvu yako, la. Mkristo mwenye hekima atajitahidi kutembea na Roho Mtakatifu ili akuze tunda la Roho na aweze kushinda tamaa za mwili. Mistari inayofuata itakusaidia kuwa na tunda zuri la uwingi. Bila Mungu hatuwezi! Mwanamke, hakikisha unamjua Mungu na tunda hili lipo maishani mwako.