#4 Wiki ya 1
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Katika Imani Yenu, tieni…
Wiki ya Kwanza: Nyumba ya Imani
Hadithi: Mama Jeni alikuwa mama mwenye raha sana. Raha yake iliwachangamsha watu wote waliokuwa karibu naye, hata kwa muda mfupi tu. Alimpokea Yesu kuwa mwokozi alipokuwa msichana na alikuwa amemtumikia Mungu kanisani tangu wakati ule. Zaidi, alifurahi kuimba na kwaya na kusaidia katika huduma ya kufanya usafi kanisani. Maisha ya mama huyo kwa kweli, yalijawa na furaha. Alienda kanisani kwa furaha na kujitolea, akishirikiana na dada zake Wakristo. Baada ya kipindi kifupi, Mama Jeni aliaanza kuumwa. Alipata ugonjwa mkali uliopunguza nguvu zake za kimwili na ya kiroho pia. Kutokana na ugonjwa huu, bosi wake alimwambia apumzike kwa muda bila kupokea mshahara. Mama Jeni alikata tamaa kwa kweli na kutokana na hali yake akashindwa hata kwenda kanisani. Alishindwa pia kusoma Neno kutokana na shida ile. Mwanzoni alijitahidi kumwomba Mungu kwa bidii, lakini kadiri ambavyo akaendelea kuugua ndivyo ambavyo akafikiri Mungu amemsahau. Wanawake kutoka kanisani kwake walimtembelea kidogo na kumwombea, lakini kila mmoja wao alibanwa na kazi nyingi na ilifikia hata wakati ambapo wakaacha kumtembelea, mara kwa mara. Mama Jeni alihuzunika sana na mara kwa mara kujiuliza, “Mungu yuko wapi? Dada zangu Wakristo wako wapi?” Baada ya kupata nafuu Mama Jeni alirudi kanisani kidogo tu. Alianza tabia ya kuchelewa kufika na kuwahi kuondoka ibadani. Vile vile aliacha kujitoa katika huduma. Siku moja Mama Rehema, dada mmoja wa kanisani, alimtembelea Mama Jeni kwa sababu alimkosa katika kwaya. Alitaka kumjulia hali Mama Jeni na alipomuuliza hali yake, Mama Jeni akamjibu kwa kusema, “Eeeh Mama Rehema, kweli siku hizi imani yangu imepotea.”
Maswali ya Hadithi: Kama imani ya Mama Jeni imepotea, je, imepotea wapi? Je, unafikiri imani inaweza kupotea? Yeye hakuenenda vizuri katika maisha yake ya kiroho kwa sababu gani? Somo: Nyumba ya Imani: Haiwezi kupotea: Soma 2 Pet. 1:3-15 Maswali ya Somo: 1.Katika 2 Peter 1:3 tumeambiwa kwamba tumepewa vitu vingapi, tunavyovihitaji kwa utauwa na uzima? 2. Kufuatana na mstari huo, je, unahitaji kuona upungufu wa kiroho maishani mwako? 3. Katika mstari wa 5 tunaambiwa tufanye nini na imani? 4. Katika mstari wa 5 hadi wa 7 Petro ametaja vitu hivyo. Sasa, wewe uvitaje vyote saba kama vilivyoandikwa.
Vitu tunavyovitia katika imani vinaweza kulinganishwa na vyombo tutiavyo nyumbani ili nyumba ipendeze zaidi. Hivyo ndivyo ilivyo na imani pia. Itapendeza zaidi tukiipamba na vyombo vifaavyo. Nyumba yetu ya Imani inahitaji vyombo. Mungu anatarajia kwamba wewe mwenyewe uvitie vyombo hivi humo. Unapohamia katika nyumba mpya, je, wewe huingia tu na kuanza kuishi bila chochote? La, kwa kawaida utachukua gari la kuhamishia vyombo vyako. Kwa nini? Ni kwa sababu nyumba yako mpya inahitaji kuwa na vyombo hivyo ili ipendeze, na bila shaka, ili wewe uweze kuishi kwa kuvitumia, au siyo? Ndivyo ilivyo na nyumba yako ya imani. Baada ya kuokoka huwezi kupumzika tu kwenye sakafu ya nyumba hiyo. Baada ya muda utachoka kulala sakafuni na kuishi maisha bila vyombo. Lazima uchape kazi kuipamba nyumba yako ya imani ili ikufae wewe kuishi humo na kuwa na maisha yenye ushindi na usalama. Kila wiki tutaipamba nyumba yetu ya imani na chombo kimoja kipya ili mwishowe tuwe na nyumba inayopendeza sana. Vilevile, ni tumaini langu kwamba wewe utakuwa na imani itakayopendeza sana. Kwa hiyo angalia sasa milingano ifuatayo ya vyombo vya kiroho na vyombo vipatikanavyo katika nyumba ya kawaida. Hii ni mfano tu utakaoweza kukusaidia kukumbuka kila sifa ya imani iliyotajika katika 2 Petro 1:5-7.
Kupamba nyumba yako ya imani kutakuwa kazi ngumu. Mungu anatutakia sisi kuwa wafanya kazi katika maisha yetu ya kiroho. Hatutaki sisi kuwa wavivu wa kiroho. Lakini habari nzuri ni hii: Mungu hajatuacha sisi kupamba peke yetu, hapana. Angalia hapo chini, Biblia inatupa sisi ahadi ya kwamba hatufanyi kazi hiyo peke yetu. Nguvu za Mungu zinatuwezesha kutia vyombo hivyo. Soma mistari inayofuata, na kisha ujibu maswali yafuatayo.
Wafilipi 4:13: Mstari huu unasema kuwa tunaweza kufanya mambo mangapi? Lakini tunayaweza tu katika nani?
Warumi 8:26: Ni nani atakayetusaidia katika udhaifu wetu? Ni nani atakayemwomba Mungu kwa niaba yetu wakati hatuwezi na hatujui kuomba vizuri?
Zaburi 105:4: Tukitaka nguvu za Bwana tufanye nini?
Dada yangu, natumaini masomo hayo yatakuhimiza kuipamba vizuri nyumba yako ya imani. Mwache Mungu akupe nguvu, mwache akupiganie nyakati ambazo huwezi. Mungu anakutakia imani iliyo imara, wala siyo iliyo haba. Mungu ameahidi kwamba wao wanaotafuta uso wake watapewa nguvu zake. Je, unataka nguvu za Mungu, ama unapendelea kutegemea nguvu zako za kibinadamu tu? Natumaini wewe utaamua leo kuutafuta uso wa Bwana Mungu wako na kutegemea nguvu zake tu! Usiwe mwanamke anayesema, “Imani yangu imepotea.” Labda imani yako si kubwa siku hizi, lakini habari nzuri kwako ndiyo hii – unaweza kukuza imani yako! Lakini huwezi kuikuza imani kama hufanyi kitu cha kuisadia ikue. Ni kazi yako kuihifadhi imani yako kwa kiasi ulicho nacho na kuifanya ile kazi ngumu ya kuipamba ili ipendeze zaidi. Wiki ijayo tutaanza kupamba nyumba yetu ya imani kwa kuweka kitanda chetu cha wema. Ubarikiwe…
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Kariri mistari hii ya somo la leo: 2 Petro 1:5b-7, Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Kila siku mpaka wiki ijayo usome 2 Petro 1:3-15 na kumwomba Mungu akufunulie vizuri maana ya mistari hii.