#3 Mwongozo wa Kiongozi
Mwongozo kwa
Kiongozi wa Masomo
“Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.” (2 Timotheo 2:15) Mwanamke Kiongozi Mpendwa, Nimefurahi sana umekubali kumtumikia Bwana Yesu kwa njia ya kuongoza somo hili kwa wanawake. Mungu akubariki kwa uaminifu wako. Ningependa kukupa mashauri na maelezo kidogo yatakayokufaa kuongoza vizuri. Nina uhakika kwamba kama una moyo wa kuongoza kundi la Biblia inamaanisha kwamba Mungu amekugusa kujitolea hivyo. Kwa hiyo najua wewe umeshafanikiwa kuwa mwaminifu mbele ya Mungu, katika mambo yote, tena mwanamke aliyeokolewa na Yesu. Wokovu ni lazima kwa kiongozi yeyote. Maisha yako yatakuwa mfano mbele ya wanawake wengine. Najua wewe unataka kuwa mfano mwema unaompendeza Mungu. Na usiwe na hofu kuwaongoza wenzako, “Mungu hajakupa roho ya woga…” Mungu anaweza kukupa nguvu kufanya kazi hiyo ukimtegemea. Kumbuka maneno ya mtumishi Paulo, “Nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Mambo yanayofuata yameandikwa kukuhakikishia kuwa uko tayari kuwa kiongozi, vilevile, yameandikwa kukusaidia na kukutia moyo. Mungu akubariki sana. Katika huduma yake, Mama Caity