#11 Wiki ya 8
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Wiki ya Nane: Picha ya Upendo
Na Katika Upendano Wa Ndugu [tieni] Upendo.
Marudio:
Sema mstari ulioukariri wiki iliyopita: Warumi 12:18 Kama umechagua siku moja katika wiki iliyopita ya kuwaonyesha watu upendano wa ndugu, toa ushuhuda wa jinsi ilivyotokea siku ile. Je, Mungu alikuwezesha?
Hadithi:
Mama Wawili aliguswa sana na mahubiri ya Mchungaji leo. Alikuwa anafundisha juu ya upendo wa Mungu. Alipoketi pale kitini akamsikiliza mchungaji kwa makini; Roho Mtakatifu alikuwa anamgusa sana.
Mchungaji alikuwa anasema, “Mungu amekupenda wewe kwa upendo mkubwa sana ingawa hujastahili kabisa kupendwa naye. Kabla hujaokoka ukamkosea Mwenyezi Mungu kwa kila namna ya kosa, ukamhuzunisha, ukamdharau, ukamwasi, ukafanya uzinzi ukafuatilia miungu na ushirikina, ukawa mbali naye, na ukawa si rafiki yake kabisa.
Hata hivyo kutokana na upendo wake wa ajabu sana akaamua kutoa mwanawe wa pekee, Yesu Kristo, aje hapa kama binadamu kukufia wewe na kukulipia deni ya dhambi zako hizo za aibu.
Hukustahili, lakini alifanya. Kwa sababu gani? Kwa sababu ya upendo wake usioweza kueleweka. Kwa upendo wake Mungu akamtoa mwanawe wa pekee ili akufie msalabani ili uweze kupata ondoleo la dhambi hizi mbaya. Mungu alifanya kila kitu. Wewe sasa umepewa kila baraka katika wokovu wako. Upendo wake Mungu ulikupa wewe nafasi ya kupatana na Mungu tena.
Lakini ndugu zangu, hayo siyo ya mwisho-- Mungu ametuambia sisi tuwe na upendo huo huo kwa watu wote. Upendo ambao utasamehe makosa ya wengine na kutupatanisha tena na watu. Upendo usio na uchoyo, bali ulio na uvumilivu na fadhili. Je, wewe unapenda watu wote na upendo huo wa kujitoa badala ya kujiombea? Je, unaonyesha upendo hata kwao waliokukosea, wasiostahili upendo wako?”
Wakati mchungaji wake alikuwa anamalizia mahubiri yake Mama Wawili alidundwa katika roho yake. Akaguswa sana na mahubiri hayo. Yeye alikuwa Mkristo aliyeokoka kwa miaka mitatu sasa. Lakini, sasa akawa anakumbuka maisha yake kabla hajaokoka na jinsi alivyofanya mengi mabaya. Akajua yeye alikuwa mmoja wa hao watu waliomkosea Mungu sana na kuwa mbali naye.
Mama Wawili akakumbuka siku zile alizopenda kuzunguka usiku na wanaume mbali mbali. Akapenda kupokea mapenzi yao. Wakati wa kufanya hivyo akakutana na kijana mmoja, Marko, aliyemvutia sana. Mama Wawili alianza kuishi naye. Kwa muda wakafurahi katika mapenzi yao, lakini baada ya muda kidogo akapata mimba. Yule kijana hakufurahi naye aliponenepa sana na mimba ya mapacha. Akamdharau sana na kumwacha mara kwa mara akienda baa.
Siku zile za zamani, alikuwa na rafiki mmoja wa karibu, Adela. Yeye akaja mara kwa mara kumtembelea Mama Wawili. Wakapendana sana na kushirikishana siri nyingi. Hata Mama Wawili akamwambia Adela juu ya uharibifu wa uhusiano wake na Marko. Adela akaelewa sana, yeye akamfariji na kumshauri sana Mama Wawili afanye mambo fulani ili kumvuta tena.
Wakati wa kujifungua Adela alikuwepo naye sana, akamletea chakula na baada ya kutoka hospitalini akamsaidia kuzoea kuwa mama wa mapacha. Mama Wawili akamshukuru Adela na akampenda sana kama rafiki yake wa karibu mno.
Marko, hakufurahishwa na wanawe; akawaona kuwa mzigo kwake. Kwa hiyo akawaondokea zaidi kwa kuwa hakufurahishwa na vilio vya watoto wake. Mama Wawili alikuwa na shughuli za kutosha na wanawe kwa hiyo hakutafakari sana juu ya desturi ya Marko ya kuondoka-ondoka.
Lakini siku moja Marko hakurudi nyumbani usiku. Baada ya kutokurudi kwa siku tatu Mama Wawili alianza kuhangaika. Akauliza majirani kama wakajua habari za Marko lakini wao hawakujua chochote. Jirani mmoja alisema, “Labda, umwulize rafiki yako, anaweza kujua.”
Mama Wawili alikumbuka hajamwona Adela kwa kama siku nne sasa. Akahangaika kidogo kwa kuwa Adela alikuwa na desturi ya kufika kila siku, au anagalau kila siku mbili. Labda angefika leo.
Baada ya wiki, Mama Wawili akahangaika sana. Hakuwaona wote wawili. Kisha jirani mmoja akapiga hodi kwake. Akaja na habari kwamba rafiki yake akawaona Adela na Marko mara kwa mara wakiwa pamoja kwenye baa fulani. Sasa akasikia kwamba wakaondoka pamoja wakapanda basi na kwenda nyumbani kwake Marko kuishi pamoja.
Mama Wawili alifadhaika sana kusikia habari hiyo. Akatamani kufa, lakini akahofia maisha ya watoto wake pasipo yeye kuwalea. Baada ya siku kadhaa, huzuni yake ikabadilika kuwa hasira na uchungu na chuki kwa wote wawili, lakini hasa kwa Adela aliyemdanganya na kumsaliti.
Baada ya wakati huo Mama Wawili alikutana na Mkristo mmoja mzuri aliyemsaidia sana kwa kumwonyesha upendo. Kwa sababu hiyo Mama Wawili akaanza kuhudhuria kanisani kwa yule Mkristo na hatimaye akaokoka. Mama Wawili akaanza kusali kwa raha na kuongezeka kiroho. Hasira, chuki, na uchungu zikapungua sana, lakini, kama Mama Wawili angesema kweli yeye hakuacha tabia hizo kwa ukamilifu. Bado zilifichika kidogo kwenye kivuli cha moyo wake.
Leo kanisani, Mama Wawili alijua kwamba Roho Mtakatifu alikuwa anamwita kuacha hisia zake mbaya na kumsamehe Adela na bwana wake. Akaenda mbele kumwomba na kumwambia Mungu kwamba atawasamehe wote wawili.
“Mungu,” akaomba kwa nia yake yote, “Nisaidie mimi kumsamehe rafiki yangu Adela na bwana yangu kama wewe ulivyonisamehe mimi ingawa mimi sikustahili kabisa. Unajua kwamba walinikosea na kuniumiza sana tena hawastahili kupokea upendo na msamaha wangu. Lakini najua kwamba upendo wako unataka msamaha. Kwa hiyo nitakutii wewe katika jambo hili.”
Mama Wawili alitoka kanisani siku ile na raha. Hatimaye kwa upendo wa Mungu yeye angeweza kuonyesha upendo.
Baada ya wiki chache tu, tangu siku ile kanisani, Mama Wawili alikuwa anaenda sokoni kununua mboga. Njiani akamwona dada mmoja aliyekuwa anatembea pole pole mtaani karibu na soko. Yule binti akawa mwembamba sana, tena akawa na dalili za ugonjwa mkali. Alipomchunguza kidogo Mama Wawili akashtuka. Yule mgonjwa alikuwa Adela, rafiki yake aliyemsaliti. Mama Wawili akashikwa na hofu ghafla. Kwa haraka kabla Adela hajamwona, Mama Wawili akaingia katika duka fulani.
Ndani ya duka akashindwa kupumua vizuri. Mawazo yake yakayumbayumba. Akaanza kuguswa na hisia zile mbaya za zamani. Lakini, papo hapo, Mama Wawili alikumbuka kumwomba Mungu. Mara moja, Roho Mtakatifu akamkumbusha jinsi alivyomsamehe Adela na kuacha hisia hizo mbaya. Mama Wawili akamshukuru Mungu akimwomba ampe upendo wa kutosha kufanya jambo gumu la kuongea naye Adela.
Alipotoka dukani akamwona Adela mbele kidogo. Mama Wawili akamkimbilia na kumwita “Adela, Adela.” Adela akageuka taratibu aliposikia jina lake. Alipomwona ni nani aliyemwita akashangaa, na hofu ikaonekana machoni mwake. Lakini Mama Wawili akamshika akianza kumkumbatia. “Adela, Adela,” akasema, “Nimefurahi sana kukuona rafiki yangu.”
Adela alianza kulia, “Eeh Mama Wawili kwa nini umenisalimia hivyo, mimi niliyekusaliti vibaya na kumuiba mume wako. Nimekukosea kweli. Naomba unisamehe. Nimeharibu maisha yako na maisha yangu pia. Marko ameniacha mimi pia na aliniambukiza yeye hali hii ya kuugua. Nimerudi hapa mjini ili kutafuta matibabu na biashara kidogo. Maisha yangu ni ya duni siku hizi.”
“Eiseee, mwanangu, hujaharibu maisha yangu,” Mama Wawili alimwambia kwa upole. “Ndiyo, mwanzoni nilifikiri hivyo. Lakini maisha yangu yamebadilika sana tangu Yesu Kristo alivyoniokoa na kunisaidia kuishi vizuri hapa duniani. Mimi naomba sasa ukubali kurudi nami nyumbani kwa muda. Nina nafasi kwa ajili yako. Utaweza kutibiwa na kupumzika vizuri. Vile vile nitaweza kukufundisha mambo mengi mazuri juu ya Mungu na upendo wake wa ajabu.”
Adela hakuweza kuamini kwamba Mama Wawili angemtendea hivyo kwa upendo mkubwa sana. Lakini aligundua kwamba mambo yote Mama Wawili aliyoyasema ni kweli. Alikubali kumfuata nyumbani. Adela hakuwa amewahi kuona upendo wa namna hii kamwe maishani mwake.
Maswali ya Hadithi:
Kama ungalitendewa na rafiki, kama Mama Wawili alivyotendewa na Adela, ingekuwaje kwako binafsi? Ungewaza nini na kufanya nini? Je, Mama Wawili alistahili upendo wa Mungu? Je, Adela amestahili upendo wa Mama Wawili na wa Mungu? Kitu Mama Wawili alichomfanyia Adela, mwisho mwa hadithi, ni kitu cha ajabu. Jaribu kueleza jinsi tendo lake lilivyoonyesha upendo halisi wa Mungu.
Somo:
Picha ya Upendo: 1 Yohana 4:7-12; 1 Wakorintho 13:4-8
Wiki iliyopita tuliipendezesha nyumba yetu ya imani na kitu kizuri sana, yaani, Kochi ya Upendano wa Ndugu. Natumai ulimwacha Mungu akupe nafasi nzuri za kuwaonyesha wengine upendano huo. Je, uliweza kumwonyesha mtu ama watu upendano wa ndugu wiki iliyopita? Usiache kufanya hivyo katika wiki zinazokuja pia.
Sasa nyumba yetu inakaribia kuwa tayari kabisa. Bado kuna chombo kimoja kinachohitajika. Naona nyumba yetu inavyo vifaa vingi sasa: kitanda, mapazia, kabati, jiko, fagio, na kochi. Lakini haiina kitu ukutani, yaani, picha. Leo tutaweka picha nyumbani. Picha ya jambo muhimu sana, yaani, Picha ya Upendo.
Maana ya upendo si rahisi kuelewa siku hizi kwa kuwa neno hili linatumika katika hali nyingi mbalimbali hata mara nyingi watu wanabadilisha maana yake iwe na maana isiyofaa sana.
Wiki iliyopita tulijifunza juu ya upendano wa ndugu. Upendano ni aina ya upendo; ni sehemu ya upendo halisi. Lakini leo tuchunguze Biblia kuelewa maana ya upendo ulio juu. Kwa lugha ya asili ya Agano Jipya, Kigiriki, upendo wa namna hiyo unaitwa “AGAPE.” Agape ni aina ya upendo uliotoka kwanza kwa Mungu. Katika somo la leo tujifunze kuwa na wanawake wenye Agape. Amina!!!
Asili ya Upendo (Agape): Soma 1 Yoh 4:7-12
Maswali ya Somo
Ms. 7 unasema upendo umetoka kwa nani? Kwa hiyo asili yake ni Mungu. Je, binadamu anaweza kuwa na upendo bila Mungu?
Watu wanaomjua Mungu, yaani wapendao, wanamjua kwa sababu gani? (ms. 7b)
Mtu asipopenda ina maana gani? (ms. 8)
Mungu alituonyesha upendo wake, hasa, katika tendo gani? (ms. 9)
Je, wewe, ulimpenda Mungu kwanza, au yeye alikupenda wewe kwanza (ms. 10)
Kwa nini mambo ya kupata “uzima kwa yeye” na “kipatanisho kwa dhambi zetu” yametajwa kuwa maonyesho ya upendo wa Mungu? Fanya mjadala ya jambo hili.
Asili ya Upendo ni Mungu
Tukitaka kukomaa katika mambo ya kiroho, lazima tuelewe kabisa umuhimu wa kazi ambayo Yesu alitufanyia sisi msalabani. Kwanza ni lazima tukumbuke jambo moja kubwa, yaani, kabla hatujaokoka sisi tulikuwa wenye dhambi tangu tuzaliwe. Sisi sote tumemkosea Mungu sana na hatukustahili uhusiano naye. Hata hatukuweza kumjua wala kumkaribisha kwa njia yoyote.
Mungu alihuzunika sana kwa jinsi vile watu walivyotengwa naye kwa dhambi zao. Sasa upendo wake unaingia. Mungu alitaka kuturudisha sisi kwake.
Alimtoa mwanawe wa pekee atufie na kumwaga damu yake kwa ajili yetu. Kufanya hivyo kulimlazimisha kujitoa kabisa kwa niaba yetu, sisi tusiostahili kabisa.
Hii ndiyo maana ya upendo; kufanyiwa kosa na mtu mwingine na kutafuta njia ya kumrudisha kwako. Maana yake ni kuziweka chini fikra zako, haki zako, kiburi chako, n.k., na kuwa na lengo moja la kumsaidia mtu yule kumjua mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
Fikiria sasa, je, kuna watu maishani mwako ambao wametengwa na Mungu na labda na wewe pia? Kwa hao wote lazima uwaonyeshe upendo huo (Agape) kwa kujisahau na kuwanyoshea mkono wako kuwasaidia kupatana na wewe na Mungu.
Inawezekana kwamba kuonyesha upendo utakugharimu. Mungu aligharamika sana. Fikiria, Baba alitoa Mwana wake na Mwana alitoa maisha yake. Gharama ilikuwa kubwa mno. Yesu alisema hivi juu ya upendo halisi:
Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake (Yoh 15:13).
Upendo Utakugharimu Dalili za Upendo (Agape): Soma 1 Kor 13:4-8
Kama upendano wa ndugu unawafanyia watu wengine wema, ndivyo ilivyo na upendo halisi. Upendo (Agape) una dalili fulani zinazouthibitisha uwepo wake maishani mwako. Katika mistari uliyosoma sasa, Paulo alitaja dalili 16 za upendo (agape). Sasa hebu mjaribu kuzitaja zote kama kundi.
Angalia dalili hizi zote tena. Je, umeshawahi kuzikamilisha zote maishani mwako?
Sasa jadiliana juu ya zile zinazowashinda ninyi. Kama kundi mjadiliane pamoja jinsi mnavyoweza kuziboresha maishani mwenu ili zianze kuonekana katika mienendo yenu.
Je, kwa nini hizi ni muhimu kuonekana maishani mwako? Je, unafikiri Yesu alizifanya zote siku hadi siku?
Sisi wakristo tumeokolewa na Mungu ili kutembea kama Yesu alivyotembea. Biblia inasema kwamba:
“Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.” (1 Yoh. 2:6)
Dada yangu, sisi tunapaswa kuishi kama Yesu mwenyewe alipotembea hapa duniani. Huna sababu ya kufanya tofauti. Mama Wawili, katika hadithi yetu ya leo, alijifunza upendo huo na aligharamika. Aliona ni juu yake kumtunza Adela kwa muda kwa upendo ili Adela apate kumjua Yesu na vilevile apate nafuu.
Na wewe je, kuna mtu yeyote maishani mwako ambaye anahitaji kuuona upendo (agape) maishani mwako. Kama yupo, mwombe Mungu akuwezeshe kumpenda na upendo ule halisi. Yule mtu hastahili upendo wako, lakini vilevile hukustahili upendo wa Mungu alipokusamehe dhambi zako na kukuokoa wewe. Kumbuka jambo hili, hustahili upendo, lakini umependwa.
Tukafanye vivyo hivyo kama tulivyofanyiwa na Mungu!
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Mstari wa Kukariri ni huu: 1 Yohana 4:10 "Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu."
Mwombe Mungu akujaze na upendo wake halisi. Anza kuwaonyesha watu wote upendo wa namna hiyo.