#10 Wiki ya 7
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Na Katika Utauwa Wenu [tieni] Upendano Wa Ndugu…
Wiki ya Saba Kochi la Upendano wa Ndugu
Marudio: Sema mstari ulioukariri wiki iliyopita:
1 Timotheo 6:6-8 Toa ushuhuda kwamba Mungu amekusaidia kuishi na utauwa katika wiki hii iliyopita.
Hadithi: Mama Gloria aliguswa sana na mahubiri alipoketi na kumsikiliza mchungaji wake. Alikuwa anahubiri juu ya upendano wa ndugu siku ile. Mwisho wa mahubiri akatoa changamoto.
“Wiki hii nawasihi ninyi kujitahidi kuishi maisha yanayoonyesha upendano wa ndugu. Mwombe Mungu akupe wewe nafasi wiki hii kuwaonyesha watu upendano huo. Nawasihi kuchagua siku moja tu katika wiki hii inayokuja kuwatendea wengine upendano wa ndugu, yaani kuwatanguliza watu wengine mbele yako.”
Mama Gloria alijua kwamba Roho Mtakatifu alimtakia afanye hivyo. Akaenda mbele ya kanisa wakati wa mwaliko kumwomba Mungu amsaidie kuwaonyesha watu upendano wa ndugu kesho, kwa siku nzima. Akatoka kanisani siku ile na raha, akafurahi kuona jinsi ambavyo Mungu angejibu ombi lake.
Jumatatu ilifika kwa haraka. Mama Gloria akaamka mapema, kama ilivyokuwa desturi yake, kuwaandalia watu wa nyumbani chai kabla hajaenda kazini.
Alipoanza kuandaa chai, akaona kwamba unga uliobaki ungetosha kwa chapati moja moja tu; ingembidi aununue baadaaye. Akafanikiwa kupika chapati na kumpa kila mmoja wa familia. Alipokuwa anapika akakumbuka ombi lake la jana. Alijiuliza, “Ni nani ambaye nitamtendea upendano wa ndugu leo?”
Mume wake na watoto walishiba na kuondoka. Yeye bado alikuwa hajanywa chai lakini akawa na muda kidogo. Kisha akasikia mtu aliyepiga hodi nyumbani kwake. Jirani mmoja, Bibi Robert, akasimama nje. Mama Gloria akaona kana kwamba alihangaika.
Bibi yule alimwambia hakuwa na unga siku ile na mjukuu wake, aliyemlea mwenyewe, angekosa chai kabla ya kwenda shuleni. Mama Gloria alikuwa na haraka na njaa na akataka kumwambia Bibi yule hawezi kumsaidia ndipo, ghafla, akakumbuka ombi lake la jana alipokuwepo kanisani.
“Bibi Robert, pole kwa matatizo yako. Ninayo chapati moja na chai kidogo imebaki, itamtosha mjukuu wako. Nitafurahi ukimpa mjukuu wako vitu hivyo ili ale kabla hajaenda shuleni.” Bibi Robert akafurahi na kusema, “Mama Gloria, nimeona kwa muda mrefu wewe ni mtu wa upendo, labda nitaenda nawe kanisani siku moja.”
Mama Gloria alifurahi pia. Akaondoka nyumbani kupanda basi na kwenda kazini. Njiani akanunua kitumbua na maji. Angalipendelea chapati na chai lakini raha yake ya kumsaidia Bibi Robert ikamtosheleza kwa njia ambayo chakula hakiwezi kumtosha mtu.
Alipofika kazini, mahali alipokuwa mfanyakazi wa ndani, Mama Gloria alimsalimia mfanya kazi mwingine na bosi wake. Baada ya muda si mrefu, aliitwa na bosi wake kuongea naye pamoja na mfanyakazi mwingine.
Bosi wao alikuwa ameshika jozi la viatu vilivyopendeza. “Naona viatu hivi havinitoshi ingawa ni vipya. Nilivinunua bila kuvijaribisha dukani. Nafikiri ninyi mtaweza kuvaa hivyo kwa hiyo amueni pamoja ni nani atakayeondoka navyo.” Mama Gloria alivutiwa sana na viatu hivyo. Alitamani sana kuondoka navyo. Lakini alipomwangalia yule mwenzake aliona hamu katika macho yake. Mama Gloria alikuwa amefanya kazi pale kwa miaka mingi kuliko huyu msichana mwingine na angaliweza kumwambia huyu kuwa anataka kwenda navyo mwenyewe. Lakini ghafla alikumbuka ombi lake la Jumapili.
“Aaah, Mungu,” aliwaza kichwani, “Mbona unanipa mimi mitihani migumu kama hii.” Lakini Mama Gloria alimpenda sana Mungu na aligundua kwamba Mungu alitaka aonyeshe upendano wa ndugu katika tukio hilo. Yule mfanyakazi mwingine hakuwa na mume, alijitegemea na alikuwa na mtoto pia. Kutokana na mawazo yake Mama Gloria alisema, “Dada yangu chukua basi viatu hivyo. Mimi sivihitaji.”
Yule dada alishangaa, kisha akaanza kulia. “Mama Gloria, siwezi kukushukuru vya kutosha. Jana viatu vyangu viliharibika kabisa. Ninazo hizi kandambili tu. Sikujua jinsi nitakavyoweza kupata viatu. Asante sana, wewe ndiwe mama mwenye upendo. Kwa nini umefanya hivyo?”
Baadaaye walipokula chakula cha mchana pamoja, Mama Gloria akapata nafasi ya kumshirikisha mwenzake habari za Yesu Kristo na wokovu. Siku ile kazini, yule dada akampokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wake wa dhambi.
Mama Gloria alifurahi sana alipotoka kazini siku ile, lakini akachoka pia. Alipoenda kupanda basi aliona kwamba basi zote zikajaa watu kituoni. Ikambidi atembee mpaka kituo kingine. Pale ikambidi asubiri nusu saa kabla hajapata nafasi ya kupanda basi. Akafurahi alipoweza kupata kiti. Lakini basi likajaa kwa haraka na baada ya muda si mrefu, basi likajaa watu sana. Ndipo akamwona mama mmoja aliyekuwa wa mwisho wa kupanda pamoja na mtoto wake aliyembeba mgongoni. Nafasi yake ilikuwa karibu kabisa na mlango wa basi. Watu wakambana huyu mama kila upande na mgongo wake uliegemea mlango kabisa. Mtoto wake akaanza kulia na mama huyu alikuwa anabeba mkoba na boxi kubwa kiasi. Alionekana kama amechoka kweli. Konda ya basi alikuwa anamsumbua kwa sababu mzigo wake ulikuwa unamsumbua yeye asifunge wala kufungua mlango vizuri.
Mama Gloria alijaribu kuangalia nje ya dirisha na kuwazia mambo mengine lakini mtoto akaendelea kulia na vilevile mama huyu akaonekana kama angeanza kulia pia, na konda akaanza kumsumbua yule mama kuomba nauli lakini alikuwa hawezi kufungua mkoba wake kwa sababu ya msongamano wa watu. Konda akaendelea kumuudhi. Mama Gloria akaanza kuguswa tena rohoni. “Mungu, kwa kweli,” akaomba, “Nimeshawasaidia watu leo na sasa nimechoka.” Lakini akaendelea kusumbuliwa na ombi lake la jana.
Kisha Mama Gloria alimtafutia nauli kwenye pochi lake, akampa konda. “Mwache sasa akamwambia” Tena Mama Gloria akamgusa yule mama. “Kaa hapa, akamwambia tubadilishane nafasi zetu.” Yule mama akashangaa na akamshukuru sana. “Mungu akubariki sana, mimi nilikuwa ninamwomba Mungu sasa hivi anisaidie. Wewe, mama, ni jibu la ombi langu.”
Mama Gloria akasimama karibu na mlango wa basi mpaka kituoni kwake lakini muda wote uliobaki wa safari yake alikuwa anamsifu Mungu kwa kumsaidia kuwaonyesha wengine upendano wa ndugu.
Aliporudi nyumbani akaona kwamba akatanguliwa na wote wa nyumbani na mtoto wake mkubwa alikuwa ameshaanza kupika. Mama Gloria akaketi kwa raha nyumbani na kuwashuhudia yote yaliyofanyika siku ile kutokana na ombi lake la Jumapili. Wote wakajengwa kusikia jinsi Mungu alivyomsaidia kuwaonyesha watu upendano wa ndugu katika siku ile. Wakagundua pia ni vizuri kama wote wangejaribu kufanya hivyo siku ifuatayo.
Maswali ya Haditihi:
Jadiliana na wengine juu ya nafasi fulani mlizowahi kupewa kuonyesha upendano wa ndugu. Ilikuwaje baada ya kumtendea mtu hivyo?
Je, kuna nyakati ambazo ulipewa nafasi ya kuuonyesha upendano wa ndugu lakini hukufanya kwa sababu ya ubinafsi au uchovu fulani?
Somo:
Kochi ya Upendano wa Ndugu: Warumi 12:10-21
Dada yangu, leo utapata kochi lako la upendano wa ndugu. Mimi hufurahi nikipata mgeni mwanamke nyumbani. Nafurahi kumkaribisha sebuleni kwangu na kuketi naye katika kochi langu tukiongea na kunywa chai. Ninapenda kochi langu sana kwa sababu inapendezesha sebule na ni mahali pazuri pa kuketi pamoja na wenzangu.
Leo utapamba nyumba yako zaidi kwa kuweka kochi yako, Kochi ya Upendano wa Ndugu. Kochi hiyo itapendezesha nyumba yako ya imani zaidi na italeta nafasi ya kujenga na kuendeleza uhusiano na wengine maishani mwako.
Soma 2 Petro 1:7 na Warumi 12:10-21:
Upendano wa Ndugu ni kwa Wakristo Wenzako.
Paulo anatuambia tupendane na upendo wa namna gani (ms. 10)? Tunawezaje, kama Wakristo, kuonyesha upendano wa ndugu?
Dalili za upendano wa ndugu ni nini (ms. 10b)? Kuwatanguliza wenzetu kwa heshima ina maana gani?
Tufanye nini kuwatanguliza? Tufanye nini kwa watakatifu? (ms. 13)
Je, unamfahamu Mkristo mwingine ambaye ana mahitaji. Umfanyie nini yule?
Upendano wa Ndugu kwa Wanaokuudhi.
Ufanye nini mtu akikuudhi, na vile vile usifanye nini unapoudhiwa naye? (ms. 14)
Katika mstari wa kumi na sita Paulo anahimiza Wakristo kupatana. Ni rahisi kupatana na marafiki, lakini si rahisi kupatana na wao wanaokuudhi. Je, upige hatua gani kuwa mpatanishi hata na wao wanaokuudhi?
Upendano wa Ndugu kwa Maadui Zako
Mistari ya 17 na 19 inatuambia tusifanye nini wakati wa kutendewa mabaya? Je, umewahi kujilipizia kisasi?
Biblia inasema tufanye nini (ms. 19b na 20)? Biblia inasema tuwafanyie nini adui wakati wa mahitaji yao (ms. 20). Jambo hili halionekani sana, lakini Paulo alisema ni dalili za Wakristo thabiti. Je, mwisho wa mstari wa 20 unasema kwamba tukiwafanyia adui zetu vema itakuwa kama tumewafanyia nini?
Tunapokutana na ubaya tufanye nini?(ms. 21)
Kumbe, maisha ya kikristo si mchezo. Kama sisi tuna nia ya kumpendeza Mungu na kubarikiwa naye inatubidi sisi kutii shauri la Neno lake. Watu wa dunia husema, “Jiangalie mwenyewe; walipizie kisasi adui zako; waache wanaokuudhi.”
Lakini Mungu anasema: “Mpendane ninyi kwa ninyi; mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi; mkae katika amani na watu wote.”
Mwanamke mwenzangu, chagua leo jinsi utakavyoenenda—kwa kufuatilia shauri la dunia, au lile lililotoka kwa Mwenyezi Mungu, Baba yako!
Mwisho, yatafakari maneno ya Yesu Kristo, na chagua kuifuata njia isiyo rahisi:
“Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:13, 14)
Chagua upendano wa ndugu kuwa mwenendo wako!
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Kariri mstari huu: Warumi 12:18: "Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote."
Kama Mama Gloria alivyofanya katika hadithi ya leo, chagua siku moja katika wiki hii kuwaonyesha watu upendano wa ndugu. Mwombe Mungu akuletee watu na kukuwezesha kuwatendea mema. Kafanye kwa kusudi.