#9 Wiki ya 6
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Na Katika Saburi Yenu [tieni] Utauwa…
Wiki ya Sita: Ufagio wa Utauwa
Marudio:
Sema mstari ulioukariri: Yakobo 1:2-3 Toa ushuhuda kama Mungu alikusaidia kuwaombea wenzako wenye dhiki au kama alikusaidia kudumu kwa saburi katika dhiki zako mwenyewe wiki hii.
Hadithi:
Mama Rehema alikuwa na mahangaiko mengi ya maisha. Mume wake akamtelekeza ili amchukue msichana mwingine akazaa mtoto naye. Mama Rehema akaachwa na watoto wawili na hakuwa na kazi. Siku hizi zilikuwa ngumu sana kwake. Mama Rehema akatafuta kazi na biashara bila mafanikio. Akahangaika sana katika maisha yake. Mama huyu alisali katika kanisa fulani ila alikuwa si mwaminifu. Watoto wake wakafurahi kusali katika Sunday School, lakini Mama Rehema alikuwa na shuguli nyingi na hakuona faida kubwa katika ibada. Kweli, hakuwa na moyo wa kuhudhuria ibada. Nyakati zile chache alizoshiriki ibada akasali na kujaribu kumwomba Mungu ampe kazi lakini bado alikuwa hajapata jibu. Kwa hiyo Mama Rehema akaona ni bora ajitegemee. Wanawake wa kanisani pale wakamkaribisha ajiunge na kipindi cha Biblia lakini hakuwa na moyo wa kukutana nao pia. Kwenye fikra zake aliwaza, "Mimi siwezi kuwaamini wanawake wengine, wanaweza wakanidanganya. Sitaki kujiunga na kipindi na sioni faida ya kujifunza Biblia zaidi. Faida ipo katika kupata ajira, hakika huyu Mungu hasikii maombi yangu siku hizi, kwa hiyo kwanini niende kanisani?”
Kwa hiyo Mama Rehema aliendelea na maisha yake magumu bila raha, bila tumaini. Siku moja jirani yake mmoja akamwambia, “Mama Rehema, naona maisha yako hayaendelei vizuri. Bora uende kwa mganga; kuna mmoja anayeitwa Daktari Pilipili, wa Sumbawanga, ambaye amewasaidia watu wengi wapate kazi. Ukimpa hela kidogo, anaweza kukusaidia, kwa hakika utapata kazi.” Mama Rehema alikuwa tayari kujaribu njia yoyote. Akamwomba ndugu yake mmoja amkopeshe hela, kisha jirani yake akamfikisha mlangoni pa Daktari Pilipili. Yule daktari alikuwa mfupi sana ila macho yake yalimtisha Mama Rehema sana. Dr. Pilipili alichukua hela zake akamwambia afanye matambiko fulani nyumbani pamoja na kumeza unga fulani uliochanganywa na maji. Dr. Pili pili akamshauri aendelee kufanya tiba hiyo kila asubuhi kwa wiki moja. “Ni dawa ya kupata ushujaa.” Pili pili alisema kwa sauti kikongwe. “Itakusaidia kuomba kazi kwa ushujaa. Dawa itaondoa hofu zako. Subiri wiki na utapata kazi.” Mama Rehema alifurahi na alifanya matambiko na kumeza dawa kwa wiki moja. Aliona ushujaa wake umeongezeka. Kisha akaenda kutafuta kazi lakini, baada ya wiki mbili za kutafuta kazi alikata tamaa tena. Hakupata kazi na sasa ndugu yake aliyekuwa amemkopesha hela alikuja kumdai. Mama Rehema alirudi nyumbani huku akilia. Kisha akajilaza kitandani na kuwasha redio yake. Hapo sauti ya uingilisti ilijaa chumbani mwake. Mhubiri alikuwa anahubiri kwa nguvu juu ya mkazo wa miujiza. Mama Rehema akavutiwa kidogo, “Mimi nahitaji mwujiza,” aliwaza mwenyewe. Kisha Mhubiri alisema kwa sauti kubwa, “Ukitaka mwujiza wako wa kazi uje kwenye mkutano wetu Ijumaa. Mungu yuko tayari kukupa kazi.” Mama Rehema aliamka kutoka kitandani kwa haraka. “Kumbe, nitaenda Ijumaa. Niko tayari kupata mwujiza wangu.” Ijumaa alienda kwenye mkutano kwa tumaini. Alipofika akaona kwamba kulikuwa na watu wengi. Mhuburi yule alikuwa anahubiri tena juu ya miujiza. Mama Rehema akamsikiliza kwa makini, alitumaini angesema tena juu ya mwujiza wa kazi ili aelewe jinsi anavyoweza kupata mwujiza huo. Hatimaye alizungumza juu ya mwujiza wa kazi, “Najua kuna watu hapa wanaohitaji kazi sana, umetafuta kazi bila kupata, mpaka umechoshwa na maisha, lakini usikate tamaa, leo ni siku yako ya kuipata. Mungu anataka kukupa wewe kazi. Uje mbele ukitaka kazi, vilevile umletee Mungu sadaka zako za shukrani kwa kazi atakayokupatia wewe."
Watu wengi kiasi walienda mbele. Mama Rehema hakuwahi kujua ni lazima kutoa shukrani kabla ufanyiwe kitu lakini alitafuta hela katika mkoba wake. Alifanikiwa kuona hela kidogo humo. Akaenda mbele na wale wengine. Akaweka hela zake katika kikapu kilichoshikiliwa na mtu wa kanisa aliyevaa nguo nyeupe, safi kabisa. “Asante dada yangu,” mwenye kikapu alimwambia, “Mungu amesikia ombi lako, sasa usiwe na wasiwasi, kazi utapata kwa hakika.” Yule mhubiri aliwaombea waliohitaji kazi. Kisha akawaambia warudi kuketi. Akaenda kuhubiri juu ya miujiza mingine, mimba, kuoana, hela, afya, n.k. Hatimaye Mama Rehema hakuvutiwa tena na mahubiri. Akaondoka kwa hamu na tumaini kwamba angepata kazi siku ile ile. Mama Rehema alisubiri nyumbani siku mbili. Hakupata kazi. “Labda nizunguke kuomba kazi,” akawaza. Alipozunguka, ikashindikana kabisa. Wiki mbili tena zikapita na hakuona hata dalili ya mwujiza wake wa kazi kutimizwa. Mama Rehema alikata tamaa sana. Alikuwa ameshapungukiwa na hela bila kupata kazi. Tumaini łąkę lilififia kabisa! Siku ile ile mama mmoja kutoka kanisani kwake alikuja kumsalimia. Mama Rehema akamfahamu kidogo kwamba alikuwa mama mzuri. Lakini kwa sababu hakwenda mara nyingi kusali kanisani hakumjua vizuri. Yule Mama Angela aliingia kwa raha. Akamsalimia Mama Rehema vizuri kwa uchangamfu na kumwambia akamkosa sana kanisani. Mama Angela alimwuliza, “Kwa nini hufiki siku hizi?” Mama Rehema alimjibu kwa aibu kidogo. “Aaah, unajua Mama Angela, shughuli zangu ni nyingi, nimebanwa sana na biashara na maisha. Sina muda wa kutosha wa kuhudhuria ibada.” Mama Angela alimshauri kwamba Mungu anataka kumsaidia lakini hatawasaidia wao wasiomtegemea. Alimwambia,“Mama Rehema, kama huwezi kuwa mwaminifu mbele ya Mungu na kuishi maisha yenye utauwa, Mungu hatakusaidia wewe sana.” “Mimi naishi maisha ya utauwa, mimi naenda kanisani.” Mama Rehema alijibu kwa hasira kidogo. “Ndiyo, unaenda kidogo, lakini hii si dalili ya utauwa. Utauwa una maana ya mtu ambaye ameokoka na sasa anataka kuishi kwa Mungu kabisa. Mwenye utauwa ataridhika katika hali yake, atajitahidi kuishi kwa Mungu siku hadi siku bila kukoma. Atakuwa na sifa ya shukrani na upendo.”
Mama Rehema aliinamisha kichwa chake kwa huzuni. Akajua kweli yeye hakuwa mtu mwenye utauwa kama alivyomaanisha Mama Angela. Aliona kwamba njia zake za kutafuta kazi zilimletea madhara mengi. Halafu, Mama Rehema akainua kichwa chake kumkazia macho Mama Angela, “Naomba unisaidie kuelewa maana ya utauwa na jinsi ninavyoweza kuupata…”
Maswali ya Haditihi:
1.Je kuhudhiria ibada za Jumapili inamaanisha mtu kuwa mwenye utauwa (mwenye hali ya kumcha Mungu)?
2. maana ya utauwa ni nini? (chagua jibu moja baadhi ya majibu yanayofuata): Ni hali ya moyo unaompendeza Mungu. AU... Ni mtu ambaye anasali vizuri na kuvaa vizuri kanisani na kusema maneno mazuri juu ya Mungu
3. Je, Mama Rehema alitafuta njia nzuri ya kupata kazi mwanzoni?
4. Je, Mganga na Mwinjilisti waliweza kumsaidia?
5. Je, Bora kama Mama Rehema angalifanya nini maishani mwake? (angalia sehemu ya pili ya 1 Samweli 2:30b juu ya kumheshimu na kumdharau Mungu.)
Somo: Ufagio wa Utauwa: Nyumba yako ya imani ni Safi?:
1 Tim 4:7-9; 1Tim 6:3-8 Nyumba inaweza kupendeza kwa nje bila kupendeza ndani. Inaweza kuwa na kuta imara, kuwa na gorofa, kuwa na mlango wa mbao mzuri, kupakwa rangi vizuri na yenye maua pembeni. Watu wanapoangalia nyumba hiyo labda wanasema, “Aisee, nyumba hii inapendeza kweli, ni nyumba nzuri sana.” Lakini kama mmoja wao aweza kuingia ndani atashangaa, yaani, nyumba ni chafu sana. Wenye nyumba hawajaosha vyombo, hawajatandika kitanda, nguo chafu zimesambaratika sakafuni, na hawajafagia wala kudeki kwa siku nyingi. Ndani yake nyumba haipendezi kabisa. Kwa kuiona nje huwezi kujua, lakini unapoingia ndani na kuona nyumba na jinsi ilivyo utasema, “nimeelewa vibaya, nyumba hii haipendezi, siyo nzuri, ni chafu kweli!” Ni jukumu la wenye nyumba ile, kutafuta ufagio na kufagia ndani. Hivyo ndivyo ilivyo katika mioyo yetu, yaani katika nyumba yetu ya imani. Mara kwa mara ni vizuri tukichukua ufagio wa Utauwa na kufanya usafi humo.
Unaweza kupendeza sana nje, na kwenda kanisani mara kwa mara, na kuongea vizuri kuhusu Neno la Mungu. Watu watasema wewe ni mwenye utauwa, yaani wewe unamcha Mungu sana. Lakini kama wangeweza kuingia moyoni mwako, je, wangehangaika, au wangefurahi? Wangeona hali gani humo, hali safi ya mtu anayempendeza na kumtii Mungu, ama hali chafu ya Mkristo anayemkosea Mungu na kuyaficha mambo hayo? Petro na Paulo walijua umuhimu wa utauwa katika maisha ya Wakristo. Waliona wanafiki wengi katika makanisa yao. Walionya Wakristo ili wakwepe unajisi na kushikilia mambo ya utauwa.
Soma: 1 Timotheo 4:7-9:
Utauwa upo kwa Upande wa Kweli “Bali hadithi za [wake]kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa…” (1 Tim 4:7-9) Kuna maneno hapo juu yenye maana sana kwa sisi wanawake. Niliangalia katika lugha ya asili ya Agano Jipya, Kigiriki, inaposema kwa Kiswahili, “hadithi za kizee.” Nilitaka ufafanuzi zaidi. Nilishangaa nilipoona katika Kigiriki maana yake ilikuwa “hadithi za wake wazee, ama za bibi.”
Maswali ya Somo:
1.Je, unajua hadithi za bibi zinazosemekana sana na kuaminika ama kufuatiliwa na watu? Haditih hizi zinapitishwa kizazi kwa kizazi. Je, kuna faida kubwa katika hadithi hizo?
2. Paulo anawaambia Wakristo kujifanya nini? (ms. 7)
3. Utauwa hufaa katika mambo mangapi (ms. 8)? Taja faida zake (angalia mwisho wa ms. 8 na mwanzo wa ms. 9). Je, faida hizo zinaweza kukufaa maishani zaidi ya hadithi (mila) za zamani?
4. Mstari wa nane unasema utauwa hufaa kwa kuleta uzima wa sasa. Maana ya uzima wa sasa ni nini?
Nimeona kuna desturi ya wanawake na wasichana katika tamaduni zote: Wote hupenda kuketi pamoja na kuongea sana (kupiga porojo) juu ya mambo ya maisha, watoto, waume, mapishi, magonjwa, nk. Mara nyingi wanawake hupenda kutoa mashauri yao katika vikao hivyo. Mashauri haya, mara nyingi, ni yale tuliyoyapata kutoka kwa akina mama na bibi zetu. Lakini mara nyingi mashauri hayo hayamfai Mkristo. Hayalingani na Neno la Mungu.
Paulo alikuwa anawaonya Wakristo wawe waangalifu sana kukataa hadithi hizo. Sisi wanawake Wakristo tunalo jukumu la kushauriwa na Neno la Mungu siyo na hadithi zisizofaa, zisizosema ukweli. Utauwa upo kinyume ya hadithi za kibinadamu. Utauwa unakumbatiana na ukweli. Ukweli upo katika Neno la Mungu.
Sisi tuwe wanawake wa Neno, si wanawake wa hadithi.
“Utauwa pamoja na Kuridhika ni Faida Kubwa.” Soma 1 Timotheo 6:3-8:
1.Kuna watu wa dini wanaofundisha vibaya Neno la Mungu. Wao hutafuta mawazo mapya na wanageuza maana nyingi za Biblia kwa maksudi yao. Je, unafahamu walimu wa namna hiyo?
2. Biblia inasema kwamba mwalimu wa namna hii ana tabia gani? (ms. 4)
3. Je, unafahamu watu wa dini/madhehebu fulani wanaopenda sana ugomvi, na ambao wanawazia habari za maswali, na mashindano ya maneno? Je, Mambo hayo yanasaidia ufalme wa Mungu? Kwa nini?
4. Waalimu wa namna hiyo wanatumia utauwa kwa njia gani? (ms. 5)
5. Paulo alifundisha kwamba utauwa wa kweli unasindikizwa na tabia gani? (ms. 6)
6. Kwa nini alisema hivyo? Kwa nini kuridhika ni muhimu kwa watu wenye utauwa?
7. Turidhike na vitu gani? (ms. 8)
Jambo hilo la kuridhika si rahisi. Paulo alisema kwamba mtu anayetaka utauwa ataridhika—basi. Nimekumbushwa hapo na Yesu aliposema katika Sala ya Bwana, “Utupe leo riziki zetu.” Riziki zetu ni chakula, nguo, na mambo mengineo. Mungu atatupa sisi hizi tukimwomba, tusijali. Tuwe na mioyo ya kumpendeza.
Mama Rehema hakujua jambo hilo. Hakuweza kuridhika na maisha yake, kwa hiyo alienda kutafuta kuridhishwa na mganga na mwinjilisti. Lakini wao hawakuweza kumtosheleza. Wao ni watu tu. Ni Mungu pekee anayeweza kututosha. Mama Rehema hakuweza kuridhika na kumtegemea Mungu; hakuelewa umuhimu wa kuwa na utauwa ndani yake.
Bila kuridhika huna utauwa kamili, na bila utauwa nyumba yako ya imani haitapendeza kwani ndani itakuwa chafu.
Uwe na Utauwa; Usiwe na Ujinga: Soma 2 Timotheo 3:5-7:
Hapo Paulo anaongea tena kuhusu hatari ya wao wanaopindua Neno la Mungu kwa maksudi yao.
1.Alisema kwamba wanao utauwa wa namna gani? (ms 5).
2. Unafikiri maana ya mfano wa utauwa ni nini? Ni utauwa unaoonekana nje tu, au ndani pia?
3. Shida ya utauwa wao ni kwamba wamekana nini? (ms. 5) Kwa hiyo, kama utauwa wa mtu upo nje tu, je huu una nguvu?
4. Paulo anaonya kwamba Wakristo wafanye nini na watu wa namna hiyo? (ms. 5)
5. Walimu wale waliteka nyara watu wa namna gani? (ms. 6) Je, unafahamu “wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi?”
6. Kwa nini ni wanawake hasa ambao huweza kudanganywa na watu wa namna hiyo (Angalia 1 Timotheo 2:13-14)?
Tumeona katika Timotheo wa kwanza kwamba tusifuate hadithi za namna za wanawake wazee. Hapa katika Timotheo wa pili tunaona kwamba sisi wanawake tusiwe wa namna ya hao wajinga. Wanawake wana udhaifu wa kuamini na kusema misemo na hadithi zisizo na maana sana.
Lakini sisi wanawake Wakristo tusiwe hivyo kabisa. Tusifuate mawazo ya kibinadamu yasiyofaa. Tusikimbilie waganga na wainjilisti bandia wanaoomba hela ama shukrani kwa msaada wao. Tuwakwepe kabisa tukimtegemea Mungu na kuridhika katika hali aliyotupa. Kama Mungu atakubali kukuponya, Yeye atafanya bure!
Chukua ufagio wako wa utauwa na uiweke kwenye nyumba yako ya imani. Fanya usafi nyumbani mwako kwa imani na kwa kukataa hadithi za wanawake wazee na walimu wa dini wasiofundisha Neno la Mungu kwa halali. Pokea Utauwa moyoni mwako. Utauwa unaofika ndani yako siyo nje tu!
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Kariri mstari huu, 1 Timotheo 6:6-8
"Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. "
Soma 1 Tim 4:7-9; 1Tim 6:3-8 kila siku wiki hii. Mwombe Mungu akusaidie kukwepa hadithi (mila) za wake kizee. Amua kuweka moyo wako kuwa na utauwa.