#8 Wiki ya 5
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Na Katika Kiasi Chenu [tieni] Saburi…
Wiki ya Tano: Jiko la Saburi (Subira)
Marudio:
Sema mstari ulioukariri wiki iliyopita: Wagalatia 5:25 Toa Ushuhuda kama Mungu amekuwezesha kukwepa kishawishi yoyote wiki hii au kuongezeka na kiasi.
Hadithi:
Mama Edithi alikuwa amejilaza kitandani kwake. Alijua kwamba anahitaji kuamka, lakini mwili wake ulikataa. Siku hizi Mama Edithi anasumbuliwa sana na ugonjwa wa sukari. Unamsumbua sana kiasi kwamba anajisikia hali ya kizunguzungu na maumivu. Bahati mbaya, katika wiki hii akakatwa mguu wake na sasa mguu ukawa unaanza kuvimba. Mama Edithi alikuwa mcha Mungu sana. Aliokoka miaka michache iliyopita na tangu siku yake ya wokovu akapenda sana kumtumikia Mungu na kushirikiana na kina mama wenzake kanisani. Wenzake wakampenda sana pia. Mara kwa mara, katika vipindi vyao vya Biblia, Mama Edithi alitoa ombi la kuombewa aponywe ugonjwa wake wa sukari. Wiki kadhaa ikaonekana kama vile Mungu amesikia ombi lake kwa kuwa ugonjwa wake ulipungua katika kuonyesha dalili zake. Lakini wiki nyingine, kama wiki hii, akaona kama vile Mungu hakusikia maombi yake. Mama Edithi alikuwa anachoshwa na ugonjwa zaidi siku hizi. Akajitahidi kudumu katika mateso yake, lakini alikuwa anaanza kukata tamaa.
Kwa hiyo, Mama Edithi alikuwa anawazia mambo hayo yote bado akiwa kitandani. Alikuwa anawaza,“Najua Mungu ananipenda, lakini kwanini hasikii maombi yangu?” Muda huo huo alipokuwa anawaza haya akasikia mtu aliyekuwa anabisha hodi mlangoni kwake. Akaamka kwa haraka ili ampokee mgeni wake. Mgeni alikuwa ni shangazi yake, Bibi Tomasi, aliyefika kumsalimia. Bi Tomasi akamsalimia kwa kusema, “Mwanangu kwanini bado umelala kitandani, vipi hali?” “Eeeh, Shangazi," Mama Edithi akamjibu, "Mimi sisikii vizuri leo asubuhi. Ni ugonjwa wangu wa sukari. Siku hizi umezidi kunisumbua.” Bibi Tomasi alitikisa kichwa chake kwa huzuni akisema, “Mwanangu, nimeshakuambia shauri langu, kwa nini hujanisikiliza? Laiti, ungalilifuata shauri langu, tayari ungalipata nafuu! Lakini, angalia sasa, jinsi ulivyo hali mbaya zaidi.” Mama Edithi alimjibu kwa uchovu, “Lakini, Shangazi, unajua mimi ninamtegemea Mungu katika tatizo hili. Neno la Mungu linafundisha kwamba tusifuate mambo ya giza kwa kushirikiana na waganga wanaofanya mambo mabaya.” Bibi Tomasi alisali katika kanisa fulani, lakini akapenda sana kutegemea mila za kabila lake, mitambiko ya kiasili. Kanisa lake likafundisha kwamba ni matendo mema ya mtu yanayomfikisha mbinguni. Yaani, siyo wokovu; pia likakwepa kufundisha mafundisho dhidi ya mila zilizopingana na Neno la Mungu. Kwa hiyo Bibi Tomasi alisema, “Mwanangu, Mungu hajakujibu bado. Labda hataki kukuponya. Sasa ni wakati wa kunisikiliza kwa kulifuata shauri langu mimi.” Mama Edithi alichoka sana. Akajitahidi kuishi na ugonjwa wake kwa subira (uvumilivu). Kila siku akamwomba Mungu ampe nguvu ya kudumu katika mateso yake. Lakini leo akasikitika, akachoka na vile vile shangazi yake akamchosha zaidi. Kwa hiyo akaanza kuwaza “Labda, nikikubaliana na shauri la Shangazi japo mara hii tu, labda yule mganga angeweza kunisaidia na Shangazi angeacha kuniudhi…. sijui…nafikiri Mungu hatafurahi… lakini, nifanye nini sasa? Nikienda kumwona faraghani wenzangu wa kanisani hawatapata kujua. Lakini kufanya hivyo si kudanganya? Ole wangu nifanye nini? Mungu nionyeshe!" Ghafla, Mama Edithi alipata jibu lake. Hapo akamkazia macho shangazi yake na kumwambia kwa ujasiri kutoka Mungu, “Eeeh Shangazi yangu, nakuheshimu kwa kuwa umenisaidia sana katika maisha yangu na ninakushukuru sana. Lakini katika jambo hili la kurudi kwa mila za kabila letu, kwa kweli mimi siwezi.
Mungu wangu amekuwa mwaminifu maishani mwangu tokea nilipompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wangu. Nimejitahidi sana kuishi ndani yake na kumpendeza siku zote. Mimi siwezi kumwumiza wala kumkosea Mungu wangu. Sijui kwanini hajaniponya, lakini ninaamini kwamba ananisikia na ataniwezesha hata wakati wa dhiki zangu. Nitaendelea kuvumilia katika ugonjwa wangu na kumwamini Mungu katika mambo yote, hata katika ugonjwa wangu wa sukari."
Maswali ya Hadithi:
1.Je, unafahamu watu waliomwomba Mungu awaponye na waliponywa naye?
2. Je, unafahamu mtu aliyemwomba Mungu amponye lakini yeye hakuwaponya?
3. Katika kumngoja Mungu, umejifunza nini katika hadithi?
4. Tusipoponywa naye, tuwe na tabia gani?
Somo: Jiko la Saburi: Warumi 5:2-4; Yakobo 1:2-4; Wakolosai 1:9a-11 Nyumba yako ya Imani imeanza kupendeza zaidi. Sasa unacho Kitanda kizuri cha Wema, Mapazia ya Maarifa, na Kabati la Kiasi. Aisee, nyumba yako ni nzuri. Naomba unikaribishe tushiriki chai pamoja siku moja. Lakini—ngoja—naona huna jiko bado. Siwezi kupata chai kwako bila kuwa na jiko la kupikia. Kwa kuwa huwezi kuchemsha chai bila jiko! Nyumba bila jiko la kupikia haifai. Wewe na familia mtakulaje? Bora upate jiko kwa nyumba yako. Leo, utapata jiko lako la saburi (subira au uvumilivu). Kama vile nyumba haifai bila jiko, ndivyo maisha yako hayafai bila saburi. Katika Agano Jipya kuna mafundisho mengi juu ya umuhimu wa saburi katika maisha ya Mkristo. Nyumba pasipo jiko haifai; vilevile maisha pasipo saburi hayafai. Pata jiko lako la saburi!
Soma Warumi 5:2-4 : Saburi Huleta Faida “Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;”
Maswali ya Somo:
1.Paulo aliwaambia Wakristo wafurahi katika hali gani? (ms. 3)
2. Dhiki ina faida gani? (ms. 3)
3. Kazi ya saburi huleta nini? (ms. 4)
Kwa kawaida watu wote, hata Wakristo, hawapendi kupatwa na dhiki. Dhiki haifurahishi. Lakini maisha ya Mkristo ni tofauti. Mungu ametuambia tutapata majaribu, na katika kitabu cha Warumi, Paulo anatuambia kwamba dhiki ni muhimu katika maisha yetu. Sababu ya dhiki si ya kutuletea madhara. Sababu ya dhiki ni kutufundisha saburi, yaani jinsi ya kuendelea au kudumu wakati wa majanga yetu. Zaidi, saburi tutakayoipata kutokana na dhiki itatuletea faida nyingine, yaani, tutapata uthabiti wa moyo. Uthabiti wa moyo utatusaidia kusimama imara wakati mashaka yanapoingia. Mama Edithi, wa hadithi yetu, alikuwa na uthabiti wa moyo. Na uthabiti huo ilitokana na saburi yake iliyosababishwa na dhiki aliyoipata kutokana na ugonjwa wake.
Soma Yakobo 1:2-4: Saburi ni Tunda la Dhiki “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali, mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.” (Yak 1:2-4)
1.Uhesabu majaribu kuwa nini? (ms. 2)
2. Furaha tupu ina maana gani?
3. Kujaribiwa kwa imani yako kunaleta kitu gani? (ms. 3)
4. Tukiacha saburi ifanye kazi yake, faida yetu itakuwa nini? (ms. 4)
Hapo Yakobo anatuambia kwamba kupata majaribu huzidisha raha yetu. Vile vile Petro alisema tusishangae tunapopatwa na mateso (soma 1 Petro 4:12, 13), bali alisema, “furahini.”
Kumbe, mambo hayo ni mazito. Mungu hajatuahidi maisha ya kustarehe; bali alituahidi uzima wa milele. Lakini hapa duniani anataka tujifunze saburi. Saburi inayotokana na njia moja tu—dhiki (majaribu, majonzi, n.k). Dhiki zinachosha, Mama Edithi alichoshwa na ugonjwa wake, lakini aliamua kudumu katika ugonjwa wake. Aliendelea kumtumikia Mungu na kuwa pamoja na wanawake wenzake. Katika mambo hayo alipata nguvu ya kuendelea na saburi.
Soma Wakolosai 1:9-11: Waombee Wenzako Wenye Dhiki “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya Mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza Kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu. Mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha;” (Kol 1:9-11).
Maswali
1.Paulo aliwaambia Wakristo wa Kolosai kwamba hajaacha kufanya nini kwa ajili yao? (ms. 9a)
2. Kwa nini ni muhimu kuwaombea wanawake Wakristo wenzetu wakati wa dhiki zao?
3. Katika sehemu ya maombi yake Paulo alimwomba Mungu awawezeshe wapate kuwa na nini? (ms 11)
4. Je, ni vema kupewa nguvu wakati wa kushindana na mateso?
5. Paulo aliwatakia wapate nini? (Mwisho wa mst. 11)
6. Kwa nini furaha inasindikiza au kuenenda na subira na uvumilivu?
Paulo alijua kwamba mateso yanachosha. Kwa sababu hiyo aliwaombea Wakristo wenzake ili wapate kuwezeshwa na nguvu za Mungu, ili wafanikiwe katika maisha yao ya kiroho. Ni muhimu sana kwa Wakristo kuombeana, hasa katika jambo la kupata nguvu wakati wa dhiki. Mama Edithi aliwapa wanawake wenzake ombi lake; vilevile, tunaweza kuwategemea wenzetu kutuombea sisi wakati wa shida. Tuombeane (Yak 5:16).
Je, wewe hukumbuka kuwaombea wanawake wenzako waliopatwa na matatizo? Je, unawaombea wajane kanisani kwako ili wapewe msaada wa Mungu kwa mahitaji yao? Je, unawaombea wagonjwa kwa uaminifu, yaani waponywe au wawe na nguvu ya kudumu katika magonjwa yao? Je, unawaombea wanawake wanaotafuta kazi/biashara, ili wawe na uwezo wa Mungu kuendelea bila kukata tamaa? Au je, unajiombea binafsi na kukumbuka mahitaji yako tu?
Lazima sisi tukumbuke kuwaombea wanawake wenzetu. Mimi najua katika nyakati za matatizo inanisaidia sana kujua kwa hakika ninaombewa na wenzangu.
Kwa hiyo katika somo la leo tumejifunza kwamba saburi (uvumilivu) inatuletea faida kubwa. Tumeona kwamba saburi ni tunda la dhiki, na wala si tunda la maisha rahisi. Na, juu ya yote, tumejifunza kuwaombea wenzetu wanaojaribiwa na mateso mbali mbali. Mungu atusaidie sisi kupata Jiko letu la saburi katika nyumba zetu za imani.
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Kariri mstari huu: Yakobo 1:2-3 Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali, mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
Soma Warumi 5:2-4; Yakobo 1:2-4; Wakolosai 1:9, 11, kila siku wiki hii. Mwombe Mungu akuwezeshe kukumbuka kuwaombea wenzako katika dhiki zao. Kisha watie moyo kwa kuwaambia umewaombea.