#2 Utangulizi/Yaliyomo
Utangulizi...
Habari,
Kitabu hiki ni cha kwanza katika mfululizo wa masomo yanayohusu wanawake haswa. Kimeandaliwa kitumiwe kwenye kikundi cha wanawake wanaotaka kujifunza Neno la Mungu na jinsi linavyowahusu . Kitabu kimeundwa kutumiwa na kiongozi mwanamke atakayeendesha kikundi katika kusoma neno na kujadiliana katika masomo. Sio lazima kwa kila mwanamke kuwa na nakala yake. Pamba Nyumba Yako ya Imani, 2 Petro 1:3-15 Imani ni jambo la ajabu. Ukimwuliza Mkristo yeyote, “Je, unapenda imani?” atajibu, “Ndiyo, napenda imani sana.” Lakini, pia, mara nyingi mwanamke Mkristo anapoanza kupata matatizo maishani mwake ataniambia, “Eeh mama, imani yangu imepungua.” Msemo huu nimeusikia mara nyingi sana. Kwa nini msemo huu umeendelea kuwa katika vinywa vyetu? Katika Biblia, Mtumishi Petro aliiona shida hiyo ya upungufu wa imani pia. Katika barua yake ya pili aliona umuhimu wa kusaidia Wakristo kuboresha imani yao. Alifundisha kwamba Wakristo wavitie vitu fulani katika imani yao. Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Katika masomo haya nimelinganisha imani yako kuwa kama nyumba iliyoimarika. Ukiwa na nyumba imara, yenye msingi mzuri, bila nyufa, yenye mabati mazuri, basi umepata kitu kizuri sana. Nyumba ya aina hii hudumu na itaweza kukulinda nyakati za mvua au za jua kali. Ni nyumba imfaayo mtu yeyote aishiye humo kwa maisha yake yote. Lakini nyumba kama hii, ingawa ni imara, haitakufaa kamili kama haina vyombo ndani yake. Ni vyema ikiwa na kitanda, kabati, mapazia, vyombo vya usafi na vya kupikia, n.k., si kweli? Hivyo ndivyo ilivyo na imani yako. Imani yako ni imara, inadumu, na inakulinda. Lakini Imani inahitaji kutiwa vyombo au sifa fulani ili ipendeze zaidi na kukufaa wewe zaidi; vyombo hivi ni kama, wema, maarifa, n.k. Masomo yafuatayo yatakufundisha jinsi ya kupamba vizuri nyumba yako ya imani. Mfano wa nyumba imara upo katika Biblia: Mithali, 14:1 inasema, “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake.” Na vile vile Mithali 24:3-4 inasema, “Nyumba hujengwa kwa hekima, na kwa ufahamu huthibitika, na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.” Dada yangu, Je, ungependa kujua nyumba yako ya imani imepambwa na vitu vyote vya thamani na vya kupendeza? Mimi nataka hivyo maishani mwangu na ninakutakia nawe pia hivyo. Najua wewe upo katika kipindi hiki cha Biblia leo kwa kuwa una moyo wa kujifunza Neno la Mungu na kujengeka kiroho. Kwa hiyo, chagua leo kuwa mwaminifu kabisa kuhudhuria kipindi hiki wiki hadi wiki. Na kati ya wiki hizi ukipewa kazi ya kufanya katika somo, ukafanye—SAWA?—Asante! Je, uko tayari kupamba nyumba yako ya imani? Twende tukaanze pamoja!