#5 Wiki ya 2
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Katika Imani yenu, tieni na Wema…
Wiki ya Pili: Kitanda cha Wema
Marudio:
-Sema mistari ulioikariri wiki iliyopita: 2 Peter 1:5b-7
-Toa ushuhuda kama Mungu alikupa nguvu zake katika jambo lolote wiki hii iliyopita ulipomtegemea yeye.
Hadithi:
Mama Jeni ni mama aliyependwa na watu wote. Yeye alijizolea sifa ya kuwa mama mwema. Alikuwa na furaha na amani katika ndoa yake kwa kuwa mume wake alimwamini kabisa na kufurahi naye. Hakika Mama huyu alijitahidi katika ndoa yake. Alimheshimu mumewe, na kujaribu kila siku kumsifu huku akimwonyesha upendo kwa njia mbali mbali. Kutokana na jinsi alivyomtendea mume wake wema, Baba Jeni alimsifia kila alikoenda. Kila alipokuwa kazini, akawaambia marafiki zake habari nzuri kuhusu mke wake. Wanaume wengine walishangaa na kutamani wake zao wawe hivyo pia.
Mama Jeni aliwapenda watoto wake sana. Kutokana na upendo huu, watoto walimheshimu mama yao. Kwa hekima alitambua kwamba watoto hawawezi kujiangalia wala kujifundisha wenyewe. Kwa hiyo yeye alichukua jukumu la kuwafundisha watoto wake mambo yanayohusu Neno la Mungu pamoja na maadili mazuri ambayo yangewasaidia watoto wake kuishi vizuri maishani mwao. Aliwafundisha kufanya kazi za nyumbani pia: usafi, kutandika, kupika, kuzoa takataka, n.k. Kutokana na mafunzo hayo waliyopata kutoka kwa mama yao, watoto wake wakasifika kuwa watoto wema.
Mama Jeni alikuwa na hekima na wema. Kila alipofungua kinywa alinena maneno mazuri tu. Kutokana na hali yake ya kuwa mcha Mungu, akatambua umuhimu wa kusoma Neno binafsi na kuomba kila siku. Alifurahi kukutana na wenzake kanisani na kujitolea kufanya huduma pale pale. Moyo wake ulitamani kumpendeza Mungu kabisa.
Sembuse na kuwa na sifa zote hizo, Mama Jeni alikuwa pia mchapa kazi. Aliamka mapema na kujitahidi mpaka usiku. Aliandalia familia yake chakula bora na kuhakikisha nyumba yake ni safi kila mara. Alijua jinsi ya kusimamia kazi mbalimbali nyumbani na aliweza kutekeleza mambo yote ya nyumbani. Alikuwa mwaminifu katika usimamizi wake kwa watu wa familia yake. Akajitahidi katika biashara mbalimbali na pesa zake zikatumika kwa hekima. Yeye alikuwa mwema wa ajabu!
Kwa kuwa alikuwa na subira, yeye aliweza kuweka akiba ya hela pembeni ili awe na amani kwa siku za baadaye. Kwa sababu ya hekima na ubunifu wake, yeye na watoto wake wakaweza kuvaa vizuri na hofu ya mahitaji ya msingi katika familia yake haikuwepo kabisa. Familia nzima ilimsifu mama huyu, na Mungu akamfurahia pia. Zipo siku ambazo Mama Jeni huchoka sana, lakini furaha yake ipo katika ujuzi kwamba familia yake itatunzwa vizuri siku hadi siku.
Maswali ya Hadithi:
-Siku hizi hakuna wanawake wengi walio wema kama Mama Jeni. Je, kwa nini yeye alifanikiwa kuwa mke mwema ingawa ni vigumu? Jadiliana mawazo yako na wengine.
Je, inawezekana kwa mwanamke yeyote kumwiga mke yule mwema, Mama Jeni? Zungumzia pamoja jinsi ambavyo unaweza kumwiga.
Somo:
Kitanda cha Wema, Je, Unacho? Soma Mithali 31:10-31
Kumbe, yule mama alikuwa mama wa ajabu sana! Mara nyingi maishani mwangu nimewahi kuisoma mistari hiyo na kukata tamaa, “Nitawezaje kuishi kama vile yeye alivyoishi?” Lakini, kumbuka mistari hii ipo katika Neno la Mungu ili itoe mfano kwetu kwa kuufuata. Kumbuka wiki iliyopita tulijifunza kwamba Mungu hatatuacha sisi peke yetu kushindana na mambo ya maisha kwa nguvu zetu pekee. Yeye atatutia nguvu zake ili tufanikiwe. Kama Mungu ametuachia sisi wanawake mfano huo wa kufuata, bora tuufuate!!
Wiki hii tunaanza kuipamba nyumba yetu ya imani. Tutaita chombo cha kwanza cha nyumba ya imani Kitanda cha Wema. Kama ilivyo vizuri kuwa na kitanda katika nyumba ya kawaida ndivyo ilivyo vizuri kuwa na wema kwenye nyumba yetu ya imani.
Mfano wa mke mwema unamaanisha aina ya wema iliyo thabiti. Kila alichofanya yeye: kuwa baraka kwa mumewe, kuamka mapema, kuchapa kazi, kusaidia watu, n.k.-- kila tendo lake lilitokana na wema wake. Lakini alipataje wema huo? Kuna sifa sita nilizoziona katika maisha yake tunazoweza kufuata na kuiga maishani mwetu: Angalia sifa hizo sita katika maswali yanayofuata.
Maswali ya Somo:
1.Kuwa Mcha Mungu: Soma Mithali 31:30 tena. Mwanamke atakayesifiwa ni wa namna gani? Soma Marko 12:30. Wanawake wengi hudai kuwa wacha Mungu lakini wangapi wanamcha kwa moyo wao wote kama Yesu alivyotuamrisha?
2. Alikuwa na Mwenendo wa Wema: Soma Mithali 31:29 tena. Je, umejulikana kuwa na mwenendo wa wema. Ndugu na Jirani zako wangesemaje juu yako na wema wako?
3. Alikuwa Mke Mwaminifu: Soma mistari 11-12 tena. Je, kuna wake wema wengi hapa duniani? Moyo wa mume wake unafanya nini? Kama umeolewa, ufanye tendo/hatua gani ili moyo wa mume wako ukuamini wewe pia? Dada yangu, kama umeolewa, umewaahidi Mungu na Mume wako ya kwamba utakuwa mwaminifu kuwa na kuishi na mume wako tu! Kwa maisha yako yote. Usijiache kuvutiwa na mwanamume mwingine kamwe! (Angalia 1 Petro 3:1-2)
4. Alikuwa Mchapa Kazi. Soma mistari 13-19 tena. Taja namna za kazi alizozifanya. Je, wewe binafsi, unafanya mambo gani ya kujiboresha ili uweze kuzidi kuwa mke mwema? Dada yangu, chapa kazi, acha uvivu, muda wetu hapa duniani ni mfupi. Yesu anaweza kukutia nguvu (Wafilipi 4:13). Tunaishi mara moja tu na maisha haya yatapita kwa haraka, kwa hiyo tuzihesabu siku zetu.
5. Alikuwa Msaidizi wa Maskini. Soma Mithali 31:20 tena. Je, unamfahamu mtu yeyote ambaye ni maskini kuliko wewe? Unaweza kufanya nini kumkunjulia mkono wako? Na kama huna kitu cha kumsaidia kimwili, umfanyie nini? Ukiangalia katika ujirani wako angalau utamwona mtu mmoja aliye maskini kuliko wewe. Umsaidie! Uwe na wema kama yule mke mwema .
6. Alikuwa Mama Mzuri. Soma mistari 21, 26 na 28 tena. Yeye aliwafanyia nini, hao watu wa nyumbani mwake(ms. 21)? Anapoongea anafanya kwa tabia gani (26)? Watoto wake wanamsema nini (ms. 28)? Je, unafanya nini nyumbani na watoto wako? Watoto wasiofundishwa na mama vizuri nyumbani watakuwa vijana wa namna gani badaaye? Watoto wengi hupotoka siku hizi, hata watoto wa Wakristo. Mke mwema alihusika katika mambo ya watoto wake (ms 21), aliwafundisha kwa hekima na sheria ya wema (ms 26). Kwa sababu hiyo watoto wake walimsifu (ms 28). Lazima uwafundishe watoto wako kwa hekima na wema ili uwakwepeshe uvivu na madhara baadaye.
Wewe mwanamke, ukijipima maisha yako kulingana na yule mke mwema, yamekuaje? Je, wewe ni mcha Mungu kweli? Je, mwenendo wako ni mwema? Je, wewe ni mke mwaminifu? Je, wewe ni mchapa kazi na msaidizi wa maskini? Je, watoto wako wataweza kukusifu siku moja?
Wema thabiti unathibitishwa na dalili zake. Dalili hizi zionekane katika maisha ya kila mwanamke Mkristo. Ukipamba nyumba yako ya imani na wema utaanza kupendeza sana mbele ya wenzako na mbele ya Mungu.
Leo fanya uamuzi, mbele ya Mungu, kujitahidi kuishi kama yule mke mwema alivyoishi. Weka Kitanda chako cha Imani humo nyumbani mwako mwa Imani.
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Kariri Mithali 31:10 na 11 "Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, wala hatakosa kupata mapato." Soma Mithali 31:10-31 kila siku wiki hii. Umwombe Mungu akufundishe na kukuwezesha kuishi kama yule Mke Mwema. Chukua kitu kimoja cha kujifunza au kuboresha maishani mwako.