#6 Wiki ya 3
Katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. (2 Petro 1:5b-7)
Na Katika Wema Wenu [tieni] Maarifa…
Wiki ya Tatu: Mapazia ya Maarifa
Marudio:
Sema mistari ulioikariri wiki iliyopita: Mithali 31:10-11 Shuhudia kama Mungu amekuwezesha kukiboresha kitu katika maisha yako wiki hii iliyopita. Je, umefanikiwa kumuiga yule mke mwema katika jambo lo lote?
Hadithi:
Mama Sofia alipiga miayo asubuhi moja, bado akiwa kitandani. Ilikuwa ni Jumapili, siku ya kwenda kanisani katika ibada. Mama Sofia alikuwa na moyo wa kusali katika ibada lakini akafurahi vivyo hivyo kuendelea kulala kwa muda kidogo. Aliendelea kulala kwa kuwa alichoka sana. Hatimaye, alipoamka akagundua kwamba alichelewa sana kwa kujiandaa. Sasa alijitahidi kujiandaa kwa haraka, lakini, kumbe, nguo zake zikawa bado hazijakauka vizuri usiku. “Eeeh, nitafanya nini?” alijiuliza. Akaenda jikoni kupika chai na akagundua kuwa sukari kumbe imeisha! Mama Sofia alimtuma binti yeke Sofia dukani kununua sukari japo kidogo. Hapo kwa redio yake walitangaza ni saa ngapi tayari. “Aiiiieeee, nimechelewa sana leo asubuhi, sitaweza kuwahi katika ibada.” Mama Sofia alihangaika kiasi. Alianza kuwaza ni kwa nini Sofia hajarudi bado. Huyu mtoto alikuwa mvivu sana siku hizi. Hatimaye, baada ya muda mrefu, Sofia akarudi kwa hali ya kutembea taratibu. Mamaye akaanza kumkemea, “Wee Sofia, unajua umenichelewesha sana, argh….Wewe ni mtoto mvivu kweli. Sasa tutachelewa katika ibada, kosa hili ni lako, kweli.” Mama Sofia alijaribu kupika chai kwa haraka na kuvaa nguo nyingine zilizokauka lakini zisizopendeza kama zile nyingine zisizokauka. Hakuwa na subira na mtoto wake, akaona kama vile Sofia alivyomchelewesha yeye na moyo wake ukapiga kwa kasi kubwa. Muda wa ibada kuanza umeshapita tayari. Hatimaye, Mama Sofia akamaliza kazi zake za nyumbani na kutoka kwake ili kuelekea kanisani.
Ndipo, mara moja, mdogo wake akafika ghafla. Wakasalimiana na kisha mdogo wake akamwambia kuwa akaja na ujumbe kutoka kwa ndugu yao mkubwa ambaye anawaita kwa kikao. Kisha mdogo wake alinyosha mikono yake kwa uchovu akisema, “Nilikuja hapa kwako kwa haraka sana; sijanywa chai bado.” Mama Sofia akawaza kichwani, “Nifanye nini sasa, niende kanisani au nimpe mdogo wangu chai. Eisee… labda ni mapenzi ya Mungu nibaki hapa leo.” Baada ya ibada, mama mmoja aliyeitwa Mama Sanura, kutoka kanisani, alifika nyumbani kwa Mama Sofia kumtembelea. Mama Sofia akafurahi kumwona. Lakini, kwa upande mwingine hakufurahi pia kumwona kwani alihisi kuhukumika moyoni kwa kutofika kanisani. Pia alimwonea Mama Sanura wivu kidogo kwa jinsi ambavyo huvaa nguo nzuri na kuwa na mume mwema. Mama Sanura alikuwa mama mwema sana. Akajitolea kanisani kila mara katika huduma akawa mhitimu wa Chuo cha Biblia. Wanawake walimpenda sana na kumfuata mara kwa mara kupata ushauri. Mama Sanura alikuwa na neno zuri la kusema kila mara na akafundisha wanawake kanisani katika vipindi vya Biblia. Mama Sofia alitamani kufanana na Mama Sanura lakini akashindwa kabisa. Ikawa ni vigumu hata kufika katika ibada za Jumapili mara kwa mara. Hakuweza kuelewa jinsi ambavyo Mama Sanura alivyoweza kufanya mambo mengi kama alivyofanya na kuyafanya vyema na kwa uaminifu. Mambo ya maisha yakambana sana Mama Sofia kila siku. Akajaribu kumwomba Mungu na kusoma neno kidogo kama alivyoshauriwa na Mama Sanura na mchungaji wake, lakini siku nyingi akaona hawezi na alipopata nafasi ya kusoma Neno la Mungu aliona kwamba hawezi kuelewa sana maneno yake.
Maswali ya Hadithi:
Kuchelewa katika ibada kulikuwa kosa la nani, la Sofia au la mama yake? Je, mnafikiri Mama Sofia anajua sana Neno la Mungu? Kwa nini? Soma Waebrania 10:12. Kufuatana na mstari huu, kama Mama Sofia angalikuwa na maarifa juu ya Neno la Mungu, je, angalichagua kumwandalia mdogo wake chai au kwenda kanisani? Kwa nini maarifa yanaweza kumsaidia mwanamke kuyajenga maisha yake vizuri zaidi? Kwa nini wanawake wengi hawataki kuchukua muda wa kusoma na kupata maarifa ya Mungu kila siku?
Somo: Mapazia ya Maarifa, Je, Unajipatia Maarifa? 2 Petro 1:5; Mithali 1:7; Mithali 2:1-12. Katika Mithali 1:7
tumeambiwa kwamba chanzo cha maarifa yote ni kumcha Mungu. Kuna watu wengi mno duniani wanaotafuta maarifa katika sehemu zisizofaa na zisizompendeza Mungu. Wanapenda sana mashauri ya binadamu kuliko yale ya Mungu. Wanatafuta maarifa katika maeneo ya ualimu, uchawi, kwa ndugu, katika mazingira, n.k.
Lakini wao wote wamekosa, hawajapata maarifa thabiti. Biblia inatuambia kwamba kumcha Mungu ni chanzo na msingi wa maarifa yote mengine.
Petro ametuambia kwamba tukitaka imani yetu ipendeze zaidi lazima tuitie maarifa pia (2 Petro 1:5). Leo tupambe nyumba yetu ya imani zaidi kwa kuweka Mapazia ya Maarifa. Mapazia yanatufaa sana kuliziba jua na kuzuia watu wasiangalie ndani usiku. Vile vile Maarifa thabiti yanaziba mawazo mabaya yasitupotoshe na kuzuia maarifa ya dunia ili yasitudanganye. Natumai, wewe, dada yangu, una moyo wa kufuatilia maarifa ya namna hii badala ya yale ya dunia. Twende tukaangalie Biblia pamoja kugundua ni wapi tunapopata maarifa hayo.
Soma Mithali 2:1-12: Asili ya Maarifa yote ni Mungu na Neno Lake. Maswali ya Somo:
1. Mstari wa kwanza tumehimizwa kufanya matendo gani mawili? Maneno ya Mungu na maagizo yake yako wapi?
2. Mstari wa pili unatushauri kufanya mambo gani mawili? Je, unafikiri ni rahisi kupata maarifa ya Mungu au ni kazi ngumu? Kwa nini?
3. Katika mstari wa tatu unatakiwa kuwa na matendo gani ili upate maarifa? Je, mtu anayetaka maarifa atayatafuta kwa juhudi kubwa au ndogo tu? Ni juhudi gani inayoonekana hapo katika mstari wa tatu?
4. Mstari wa nne unasema maarifa yana thamani kubwa na tufanye nini ili tuyapate? Kama ungesikia kwamba hazina ya sarafu za dhahabu zimefichwa mahali fulani, je, ungefanya nini?
5. Angalia mstari wa tano. Tumeahidiwa nini tukifuata shauri la Mungu kwenye mistari 1-4? Ukifanikiwa kumjua Mungu zaidi, itajulikanaje katika maisha yako?
6. Soma mistari 6-12: Maarifa Thabiti Huleta Faida. Katika kundi lenu, tajeni faida zote za maarifa mnazoziona katika mistari hiyo. Mimi nimezihesabu faida kumi na tatu, na ninyi, je?
Unaweza kuona jambo lingine pia—Maarifa hayatawasili kwako ghafla. Unahitaji kuyatafuta kwa bidii. Njia ya kupata maarifa si rahisi. Je, inasema hapo, “Ukilala kitandani ujuzi utakudondokea ghafla?” Hapana! Haisemi hivyo. Au inasema hapo, “Ukienda kwa mganga, yeye ataweza kukuambia maarifa yanayofaa?” Hapana! Haisemi hivyo! Au inasema hapo, “Ukimkimbilia jirani yako wakati wa shida yeye atakuwa na ujuzi mzuri wa kukusaidia?” Hapana! Hata haisemi hivyo, “Ukisoma mpaka uhitimu chuo kikuu na kupata shahada ya PhD, utakuwa na maarifa ya juu.” Hapana! Maarifa hayapatikani kwa urahisi. Angalia mstari wa tano: “Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, na kupata kumjua Mungu.” Eeeh dada, je, unataka kuwa mcha Mungu? Je, unataka kumjua Mungu? Biblia hapa inatuonyesha kwamba njia pekee ya kumcha na kumjua Mungu ni kwa kulishikilia Neno lake Mungu. Usiridhike na upungufu wa maarifa maishani mwako. Uyatie maarifa katika nyumba yako ya imani. Tukifanya kazi ngumu ya kupata maarifa (busara, ujuzi, n.k.) tutabarikiwa kwa kupata vile tulivyovitafuta. Tutapata busara, ulinzi kamili wa Mungu, haki, hukumu, akili, njia njema, maarifa, ufahamu, n.k. Dada yangu, je, unataka hayo? Kama umejibu ndiyo nina neno moja tu kwako—UKAFANYE! (Shauri kwa Kiongozi: ukipendelea, maliza somo hapa na endelea wiki ijayo na lile lifuatalo. Kama umefanya hivyo, soma hadithi ya wiki hii tena ili wanawake waikumbuke. Fanya marudio ya sehemu ya kwanza ya somo hili pia.)
Soma Yeremia 23:25-29: Hapo zamani katika nchi ya Israeli kulikuwa manabii bandia wasiotumwa na Mungu. Lakini watu wengi walipendelea kuzisikiliza habari za ndoto zao kuliko kusikiliza Neno la Mungu kama lilivyotabiriwa na manabii halisi kama Yeremia. Je, siku hizi umewahi kusikia habari za watu wanaovutwa na kuathiriwa na ndoto zao au za wengine?
Soma mistari 25-26. Mungu anaongea juu ya manabii hao wanaofundisha ndoto zao, hata kwa jina lake. Unafikiri Mungu amefurahi nao? Wale manabii wanajaribu kuwafanya nini watu wa Mungu (ms. 27)? Siku hizi kuna watu wanaojaribu kufanya hivyo kwa makusudi yao? Zungumza pamoja juu ya madhara ambayo watu wale wanaleta katika mwili wa Kristo. Katika mstari wa 28 unafikiri makapi yanalingana na nini na ngano na nini? Hapo Yeremia anatuambia kwamba tusiweke imani yetu katika ndoto. Ndoto ni kama makapi, yaani, hayafai kuwa chakula. Neno la Mungu ni kama ngano, yaani, linatufaa kabisa. Kwenye mstari wa 29, Mungu anafananisha Neno lake na nini (vitu viwili)?
Dada mpendwa, usivutiwe na ndoto na maneno ya watu, hata maneno ya watu kiasi fulani wanaojiita watumishi wa Mungu. Kama ndoto au maneno yao hayalingani na Neno la Mungu, ndoto na maneno hayo ni uongo. Weka maisha yako, imani yako, na kazi zako zote ziwe na nia moja ya kulijua Neno la Mungu.
Faida ya Maarifa:
Tutamjua Mungu na kuweza kumcha Yeye.
Tutakuwa na hekima, yaani, tutaweza kuwa na uwezo wa kuelewa na kutatua mambo magumu katika maisha yetu.
Tutaweza kuwashauri watoto wetu na wengine.
Tutakuwa na ujuzi wa jinsi ya kumjibu mtu vizuri.
Tutaweza kuyaunda maisha na ratiba zetu vizuri.
Tutaweza kumtumikia Mungu zaidi kanisani.
Tutakuwa na hamu ya kupata elimu zaidi (Masomo ya Biblia, Chuo cha Biblia, semina za Kikristo, n.k.)
Utakuwa mwaminifu na watu wataliamini neno lako zaidi.
Kazi ya
Kufanya Wiki Hii:
Kariri Mithali 1:7: "Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu."
Soma Mithali 2:1-12 na Yeremia 23:25-29 kila siku.
Umwombe Mungu akupe hamu na nia ya kupata maarifa zaidi. Tafuta njia moja wiki hii ya kujipatia maarifa ya Mungu zaidi.